Habari
MHANDISI MAHUNDI ATOA MWEZI MMOJA KWA TTCL KUBORESHA HUDUMA ZA INTANETI MPAKA WA KASUMULU

Na Mwandishi Wetu, WMTH Mbeya
Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb.), ameziagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na makampuni ya simu kufanya uhakiki wa huduma za mawasiliano katika eneo la mpaka wa Kasumulu, ili kuondoa changamoto ya wakazi wa eneo hilo kupokea mawasiliano kutoka nchi jirani badala ya mitandao ya Tanzania.
Naibu Waziri Mahundi ametoa maelekezo hayo Machi 20, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika eneo la Kasumulu, Mbeya mpakani mwa nchi ya Tanzania na Malawi.
“Sisi kama Wizara tungependa kuona wananchi wetu wanaoishi mipakani wanafurahia huduma bora zinazotolewa na taasisi zetu. Serikali ya Rais Samia imewekeza sana katika sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za uhakika,” alisema Mhandisi Mahundi.
Aidha, Mhandisi Mahundi amelitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mkoa wa Mbeya, kuongeza nguvu katika huduma za intaneti za mkongo Taifa wa Mawasiliano katika eneo hilo la mpaka, ili kuhakikisha upatikanaji wa intaneti yenye kasi na kuimarisha huduma kwa wananchi na wafanyabiashara wa mpakani.
“Tunataka kupitia fedha anazozitoa Mhe. Dkt. Samia, Watanzania wanufaike na mawasiliano ya uhakika ya ndani ya nchi. Mtu atumie mawasiliano ya nje ya nchi pale tu anapokuwa nje ya nchi au kwa hiari yake, na si kwa kulazimika kutokana na changamoto za mitandao ya ndani,” alisisitiza Mhandisi Mahundi.
“Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mahundi ameipongeza TBC Taifa na Bongo FM kwa kuweka mitambo ya kurushia matangazo katika eneo hilo la mpakani kupitia ruzuku waliyopewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Vilevile, Mhandisi Mahundi amewataka watoa huduma za mawasiliano kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano kwenye maeneo ya vivutio vya utalii, ili kuchochea shughuli za sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Awali, akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Forodha wa Mkoa wa Mbeya, Nasibu Kalombola, alisema kasi ndogo ya mtandao katika eneo la mpaka wa Kasumulu ni changamoto kubwa, huku muingiliano wa mawasiliano kutoka nchi jirani ukiathiri upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa eneo hilo.