Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MHANDISI KUNDO AZINDUA DUKA LA POSTA MTANDAO


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa Duka Mtandao la Posta ulioambatana na Maadhimisho ya Wiki ya Posta kuelekea Siku ya Posta Duniani katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma

 

DODOMA

*Duka mtandao kuwezesha biashara mtandao

*Wajasiriamali 428 wajiunga na duka mtandao la Posta

*Duka mtandao kufanikisha wajasiriamali kuuza na kununua bidhaa nchini na duniani kote

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amezungumzia huduma ya duka la posta mtandao kuwa ni moja ya ubunifu wa biashara uliofanywa na Shirika la Posta Tanzania ikiwa ni matokeo ya kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)

Mhandisi Kundo amezungumza hayo leo tarehe 06/10/2021 akizindua rasmi duka la posta mtandao jijini Dodoma ikienda sambamba na uzinduzi wa maonesho ya Wiki ya Posta kuelekea Siku ya Posta duniani itakayofanyika tarehe 9/10/2021

Amesema kuwa kupitia duka la posta mtandao wajasiriamali na wafanyabiashara waliopo nchini wataunganishwa na masoko ya biashara na bidhaa zao pote duniani kupitia matawi ya Shirika la Posta yapatayo 670,000 duniani pote na matawi 350 ya Shirika la Posta yaliyopo ndani ya nchi

“Duka la Posta Mtandao limedhihirisha kwa vitendo ufanisi mkubwa kwa watendaji wa Wizara na taasisi katika kutafsiri Sera ya TEHAMA na kuleta mapinduzi makubwa ya teknolojia ya dijitali katika utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao”, amezungumza Mhandisi Kundo

Amesema kuwa ubunifu uliofanywa na Shirika hilo umeleta mapinduzi makubwa ya kuuza na kununua bidhaa pote duniani ambapo mpaka sasa wajasiriamali wapatao 428 nchini wamesajiliwa na duka hilo

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Wizara hiyo na taasisi zake inatembea na kauli mbiu ya kutembea pamoja na kazi yao kubwa ni kuweka miundombinu itakayoifikisha nchi kwenye uchumi wa dijitali kupitia Wizara hiyo na taasisi zake 8

Amesema kuwa kuna mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia Shirika la Posta Tanzania mojawapo ni kupata uwakilishi wa mabaraza mawili ya Umoja wa Posta Duniani ambayo ni Mjumbe wa Baraza la Utawala na Mjumbe wa Baraza la Uendeshaji wa Posta Duniani wenye jumla ya nchi wanachama 192

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabir Kuwe amesema kuwa Shirika la Posta limeonesha kuwa teknolojia ni fursa kwa mabadiliko makubwa yaliyoonekana baada ya Shirika hilo kuanza kutumia teknolojia kutoa huduma zake ambapo mpaka sasa jumla ya leseni 119 zimetolewa na TCRA katika Sekta ya Posta

Kaimu PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrise Mbodo amesema kuwa Shirika la Posta la sasa ni zaidi ya kutuma na kupokea barua na kuwataka wananchi kujiunga na duka la posta mtandao kupitia kikoa cha www.postashoptz.post ambapo mpaka sasa maduka 128 yameshajiunga

Amezianisha sifa kubwa za duka mtandao la posta kuwa limeunganishwa na mtandao wa posta pote duniani, linatumia lugha zaidi ya 20, lina huduma za usafirishaji  wa haraka na wa njia ya kawaida, uhakika wa masoko ya ndani na nje ya nchi na asilimia 97 ya mauzo inabaki kwa mfanyabiashara au mjasiriamali na asilimia 3 tu ndio inabaki kwenye Shirika la Posta.