Habari
MFUMO WA LOIS WA EWURA UMEUNGANISHWA NA MFUMO WA UTAMBUZI WA NaPA
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.
Wataalam wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) wanaendelea na kazi ya kuunganisha mfumo wa kielektroniki wa Anwani za Makazi wa NaPA na mfumo wa LOIS wa EWURA.
Mfumo wa LOIS ni mfumo wa kielektroniki wa maombi ya leseni za Umeme, Mafuta na Maji na huduma nyingine zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo ambapo kwa kuunganishwa na mfumo wa NaPA utawarahisishia wakaguzi na watumiaji huduma hizo kuweza kuvifikia vituo vinavyotoa huduma za nishati na maji kwa urahisi.
Mtaalamu wa mfumo wa NaPA kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Anorld Mkude amesema mfumo wa NaPA unafungua fursa za uchumi wa kidijitali kwa kuboresha utoaji na upokeaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.
Bw. Mkude amezungumza hayo akitoa wasilisho wakati wa kikao cha Wizara hiyo na EWURA kilichofanyika tarehe 01 Oktoba, 2024 katika ofisi za Makao Makuu ya EWURA jijini Dodoma ambapo amesema mpaka sasa takribani mifumo 12 ya kisekta inasomana na mfumo wa NaPA ikiwa ni pamoja na mfumo wa LOIS.
Naye Mkaguzi wa Petroli wa EWURA, Mhandisi Ibrahim Kajugusi amesema kazi inayoendelea katika kuunganisha mifumo hiyo ni pamoja na kusasisha taarifa ili kuhakikisha taarifa za NaPA na LOIS zinafanana.
Ameongeza kuwa mfumo wa NaPA utawarahisishia wakaguzi kutoka katika Mamlaka hiyo pamoja na watumiaji wa huduma kuweza kuvipata na kuvifikia vituo vya mafuta vilivyopo katika maeneo yao.
Naye Mratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Jampyon Mbugi amesema kuwa usajili wa Anwani za Makazi ni endelevu kwa wataalamu kufika eneo husika na kufanya usajili ili kuepuka mfumo kuwa na taarifa chafu.
Ameongeza kuwa siku zijazo mfumo utaruhusu mtu kusajili mwenyewe Anwani kwa njia ya mtandao lakini kwa vigezo maalumu ili kuepusha taarifa zisizo sahihi kuingia kwenye mfumo huo ambao unarahisisha utambuzi wa wakazi na makazi.