Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI KUCHOCHEA UCHUMI WA KIDIJITI


na TAGIE DAISY MWAKAWAGO, WHMTH

         Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ina mengi ya kujivunia katika kusherekea Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika) ambapo mapinduzi makubwa yanayofanyika katika sekta ya Mawasiliano na Teknolojia kwa ujumla yamechochea maendeleo kwa wananchi na kuifanya Sekta kuwa moja ya sekta bunifu katika kufanikisha Tanzania kuwa na uchumi wa kidijiti.

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) duniani ambayo kwa sasa hayaepukiki, nayo pia yamewezesha wataalamu kutumia ujuzi wa kidijitali na kuvumbua mifumo ya kielektroniki inayorahisisha ufikishwaji wa huduma mbalimbali kwa  wananchi ikiwa pia ni utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26. Utekelezaji wa Mpango huu unaifanya sekta ya Mawasiliano kuwa moja ya sekta za kipaumbele nchini. Katika kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, Mfumo wa Anwani za Makazi “National Physical Addressing System – NaPA” ulibuniwa ili kufikisha huduma mbalimbali za kijamii kwa urahisi na wakati kama vile biashara za mtandao, utumaji wa barua, nyaraka na vipeto nyumbani,  ofisi mbalimbali na maeneo ya biashara.    

Mfumo huo unaotumia miundombinu ya kidijiti utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 ambapo bado ni endelevu kutokana na zoezi la kusasisha taarifa mbalimbali linaloendelea nchi nzima. Mfumo huo unasaidia utambuzi wa maeneo halisi, jina la barabara, mitaa au kitongoji/ Shehia; taarifa za wamiliki wa anwani na majengo husika; utambuzi wa huduma kadhaa zinapopatikana au kitu cha huduma kilipo; na unatambua postikodi ya eneo/kata husika.  Aidha, mfumo huo wa NaPA umeunganishwa na mifumo mingine hususan kwenye sekta za ardhi, usajili wa leseni za biashara, Mamlaka ya Kodi; pamoja na Vitambulisho vya Taifa.  

Mapema mwezi Februari 2022, Wakuu wa Mikoa walifanya operesheni maalum ya utambuzi wa anwani katika maeneo yao kufuatia maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alielekeza anwani hizo zipangwe kwa muktadha wa tarakimu za eneo, majina ya barabara, mitaa, namba za nyumba, ofisi au majengo. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha anwani zinatambulika rasmi katika kumbukumbu na mifumo ya Serikali ili huduma zote za kijamii ziweze kuwafikia wananchi popote walipo kwa urahisi kupitia usafirishaji, posta au huduma za ana kwa ana.  Operesheni hiyo ilikamilishwa kwa asilimia 95 mwezi Mei 2022 katika ngazi za kata, wilaya, mikoa na kanda kutoka asilimia tatu mwaka 2021.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa wakati wa operesheni maalum ya Anwani za Makazi takwimu zinaonesha kuwa idadi ya barabara/mitaa iliyotambuliwa ni 329,507; idadi za anwani zilizokusanywa ni 12,385,956; huduma na biashara zilizotambuliwa 675,668; wakati idadi ya anwani zenye majengo ni 12,011,576.  Utambuzi huo pia uliwezesha zoezi la Sensa ya majaribio kufanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kufanya Sensa ya Majaribio (Pilot Census). Matokeo ya zoezi hilo yalihamasisha ukamilishaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi katika kuweka mazingira wezeshi ya utambuzi mbalimbali wa maeneo ya makazi, biashara, majengo, miji na vijiji wakati wa kuelekea kwenye Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti 2022.

         Aidha, Mfumo wa Anwani za Makazi pia unaendana na azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa kidijiti kwa kurahisisha matumizi ya kielektroniki kuwa rafiki kwa mtumiaji ili kukidhi mahitaji ya kijamii.  Huduma hizo ni pamoja na uwezeshwaji kwa mteja kuhakiki taarifa binafsi au za ndugu, jamaa na rafiki kuhusu anwani za makazi na biashara; uwezeshwaji wa kutumia anwani katika kusajili kadi za benki, kufanya biashara mtandaoni, n.k.

WHMTH ina mengi ya kujivunia katika kusherekea miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika) kwa kuchangamkia fursa zinazotokana na mapinduzi ya teknolojia kupitia programu tumizi ya kidijiti ya NAPA yenye kutunza taarifa za Anwani za Makazi inayowezesha pia ufikishwaji wa huduma kwa urahisi popote alipo mwananchi.. Faida nyingine zinazotokana na matumizi ya  Mfumo huo ni pamoja na huduma za, usafirishaji, afya, zimamoto, , uchaguzi, pamoja na masuala ya uhamiaji. Ili kuwa na matumizi ya Mfumo yenye ufanisi kwa jamii, kuna umuhimu wa kufanya maboresho katika Sheria na Kanuni zinazotumika kwa sasa ambazo ni Tanzania Buildings Agency (Establishment) Order, 2003; The Executive Agencies (The Tanzania National Roads Agency) (Establishment) Order, 2000; Sheria ya Wakala wa Barabara Zanzibar Na. 11/2019; The Electronic and Poastal Communication Act of 2010; The Roads Act of 2007; Electronic and Postal Communication (Postal) Regulations, 2018; na The Executive Agencies (Tanzania Rural and Urban Roads Agency) Establishment Order, 2017.

         Kutokana na ukosefu wa Sera na Sheria ya Anwani za Makazi, WHMTH bado imeweza kutekeleza malengo ya Serikali ya kuwa na mfumo huo kupitia Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003; Makubaliano ya Umoja wa Posta Afrika na Umoja wa Posta Duniani; na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025.  Ni mategemeo kuwa wananchi wataendeleza tamaduni za kusasisha taarifa zao za Anwani za Makazi ili kuendana na huduma mbalimbali zitakazohitaji taarifa hizo. 

Katika kuazimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni dhahiri kuwa imepiga hatua kubwa ya mabadiliko katika utoaji na ufikishaji wa huduma za Habari na Mawasiliano nchini.  Mabadiliko hayo ambayo yanatokana na ukuaji wa teknolojia yamejenga hamasa kwa Wizara katika kuhakikisha kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi unakuwa chachu ya kuchochea uchumi wa kidijiti kwa kuunganishwa  kikamilifu na mifumo mbalimbali inayotoa huduma kwa jamii.  Dhana kuu ni kuhakikisha kuwa Wizara na Taasisi zake zinaendelea kubuni mikakati endelevu ya mifumo ya TEHAMA ambayo ni rafiki, shindanishi na inayoendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kusherekea miaka 61 ya Uhuru itaendelea kubuni mifumo yenye kutoa huduma zinazoendana na Mapinduzi ya 4 ya Viwanda, ili wananchi wazidi kunufaika na huduma za mawasiliano kupitia mazingira wezeshi ya teknolojia ya kisasa.