Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YASHIRIKI MKUTANO WA 18 KIMATAIFA WA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU


Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeshiriki katika Mkutano wa 18 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu unaoendelea nchini Marekani katika Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa uliopo New York.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi maalum Bw. Amon Mpanju ambapo Wizara ya Mawasiliano na teknolojia ya Habari imewakilishwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamuzi wa Rasilimali Watu Bi. Salome Kessy (mwenye koti la pinki) na Afisa TEHAMA Mwandamizi Bw. Khalid Nyange.

Aidha, ujumbe wa Tanzania ulikuwa na uwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo Mkurugenzi Msaidizi wa Makundi Anuai ya Jamii, Bi. Mwanaamani Mtoo ameshiriki mkutano huo.

Moja ya mada zinazojadiliwa katika majukwaa mbalimbali yanayofanyika katika Mkutano huo ni pamoja na ushirikishwaji na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika matumizi ya Akili Unde, sambamba na kuangazia haki na wajibu wao katika ujumuishwaji wao.

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kutekeleza Mradi wa Tanzania ya Kidijiti (DTP) ambapo moja ya maeneo muhimu ya utekelezaji ni ujumuishwaji na ushirikishwaji wa makundi anuai wakiwemo watu wenye ulemavu katika mapinduzi ya kidijiti nchini.