Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MAWASILIANO YA INTANETI YABORESHA SHUGHULI ZA UTALII NGORONGORO


Na Mwandishi Wetu,WHMTH,  NGORONGORO.

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma za kidijitali nchini ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro kupata intaneti yenye kasi ya 4G.

Hayo yamebainishwa na Mhandisi Kelvin Mwakaleke wa Wizara hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya mawasiliano inayotekeleza chini ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali iliyofanywa tarehe 30 Agosti 2024 katika hifadhi hiyo.

Mhandisi Mwakaleke amesema awali mnara huo wa Tigo uliojengwa kwa ruzuku ya Serikali ulikuwa unatumia teknolojia ya 2G na baada ya  kupandishwa hadhi unatoa mawasiliano ya intaneti yenye kasi ya  4G. 

Naye Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA wa Wizara hiyo Bw. Mohammed Mashaka anayesimamia Mradi wa Tanzania ya kidijitali, amesema lengo la kuupandisha hadhi mnara huo ni kukuza uchumi wa kidijitali kupitia sekta ya utalii.

Amefafanua kuwa mnara huo kupandishwa hadhi ni sehemu ya utekelezaji wa mikataba iliyosainiwa mwezi Mei 2023 baina ya Serikali na kampuni za simu ya ujenzi wa minara 758 na kupandisha hadhi minara 304. 

Kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka Benki ya Dunia, Bw. Paul Seaden amesema kuwezesha upatikanaji wa huduma ya intaneti ya 4G katika maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro ni matokeo chanya ya mradi huo kuchangia ajenda ya maendeleo katika sekta ya utalii.

Naye Mratibu wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Bakari Mwamgugu, amesema kupitia mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia eneo la hifadhi ya Ngorongoro mbali na kuwezeshwa mawasiliano ya intaneti pia litawekewa mfumo wa Anwani za Makazi ili kuboresha shughuli za utalii katika eneo hilo.