Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MAWASILIANO KUIMARISHWA MIPAKANI, TARIME NA RORYA KUNUFAIKA


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (akizungumza na wananchi katika kata ya Mwema Wilaya ya Tarime wakati akikagua upatikanaji wa huduma ya Mawasiliano katika Kata hiyo

 

MARA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa moja ya vipaumbele vya Wizara hiyo ni kuimarisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuinua uchumi wa nchi

Akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mara na kutembelea Wilaya ya Tarime na Rorya amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepanga kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kupeleka mawasiliano katika Kata 11 za Wilaya ya Tarime na kiasi cha shilingi Milioni 290 katika kata 2 za Wilaya ya Rorya ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022

Aidha, Mhandisi Kundo amefika katika kata ya Ikoma na kata ya Bukura ulipo Mpaka wa Kirongwe wilayani Rorya na kukuta hakuna mawasiliano kwa upande wa Tanzania na kupelekea wananchi wa kata hizo kutumia roaming ya Safaricom ambao ni mtandao wa nchi jirani ya Kenya

“Ziara yetu sio ya kuona na kuondoka bali tunachukua hatua maeneo yenye changamoto kwasababu ni jukumu letu kuwafikishia wananchi huduma ya mawasiliano hili la watanzania kutumia mtandao wa nchi jirani sio sahihi kwasababu mbali na kutumia gharama kubwa kuwasiliana kupitia roaming pia wanalipa kodi nchi nyingine” amesema Mhandisi Kundo

Ameongeza kuwa Kata ya Ikoma na Bukura hazipo kwenye orodha ya kupelekewa miradi ya mawasiliano ndani ya mwaka wa fedha 2021/22 lakini wamejadiliana na wataalam alioambatana nao na kuamua kata hizo mbili zitapelekewa huduma ya mawasiliano kwa mpango wa dharura tofauti na utaratibu wa kawaida

Maeneo mengine ambayo yamewekwa kwenye mpango wa dharura wa kupelekewa mawasiliano ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Rorya na kwa upande wa Wilaya ya Tarime ni katika lango la lamai la kuingilia hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime Luteni Kanali Michael Mtenjele amesema kata 11 za wilaya hiyo kupelekewa huduma ya mawasiliano ni hatua muhimu ya kuimarisha ulinzi na usalama katika wilaya hiyo hasa inapotokea dharura yeyote mpakani mawasiliano yatasaidia maafisa waliopo mpakani au wananchi kuweza kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo Makao Makuu ya Wilaya kwa ajili ya msaada

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Juma Chikoka ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa maamuzi waliyochukua ya kupeleka mawasiliano katika Wilaya hiyo kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma ya mawasiliano na mtandao ambapo kukosekana kwake kunasababisha ufinyu wa makusanyo ya mapato ikizingatiwa kuwa mashine za posi zinazotumika kukusanyia mapato zinatumia mtandao lakini pia ni mawasiliano ni muhimu ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya mipakani