Habari
MATUMIZI YA PESA MTANDAO YAFIKIA TRILIONI 640.2
Na Mwandishi wetu, WMTH Dodoma
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), amesema Sekta ya Mawasiliano imeendelea kukua kwa kasi na kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa kidijitali, huku thamani ya miamala ya fedha kupitia simu za mkononi ikifikia Shilingi trilioni 640.2 katika mwaka wa fedha 2025/26 kutoka Shilingi trilioni 214.6 mwaka 2021/22.
Akiwasilisha taarifa ya Mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano na Takwimu za Sekta ya Mawasiliano mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Dkt. Mkama alisema ongezeko la Shilingi trilioni 425.6 ni sawa na ukuaji wa asilimia 198 katika kipindi cha miaka mitano. Aidha, aliongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za pesa mtandao pamoja na kuimarika kwa ujumuishaji wa kifedha na kidijitali nchini.
Vilevile, alieleza kuwa idadi ya miamala iliyofanyika kupitia mifumo ya pesa mtandao imeongezeka kutoka miamala bilioni 4.08 mwaka 2021/22 hadi kufikia miamala bilioni 10.09 mwaka 2025/26. Huduma ya M-Pesa imeendelea kuongoza kwa kusajili miamala bilioni 3.4 katika kipindi hicho, ikifuatiwa na Mixx by Yas yenye miamala bilioni 2.94 na Airtel Money yenye miamala bilioni 2.50.
Kwa upande wa matumizi ya Intaneti, Mhe. Dkt. Mkama alisema kiwango cha data kilichotumika nchini kimeongezeka kwa kasi kutoka Gigabyte milioni 446 mwaka 2021/22 hadi Gigabyte bilioni 2.48 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 456. Alisema hali hiyo inaonesha kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mtandao katika biashara, elimu, mawasiliano na utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa njia ya kidijitali.
Kwenye eneo la mapato, Sekta ya Mawasiliano imeendelea kuimarika ambapo mapato ghafi ya kampuni za simu yaliongezeka kutoka Shilingi trilioni 2.94 mwaka 2021 hadi Shilingi trilioni 5.57 mwaka 2025. Aidha, Mhe. Dkt. Mkama alisema takwimu hizo zinaonesha mchango mkubwa wa Sekta ya Mawasiliano katika kukuza uchumi wa taifa na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
