Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MATUMIZI SALAMA YA MTANDAO YASISITIZWA KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI NCHINI


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Mwanza.

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetoa wito kwa wanafunzi wa shule za sekondari kutumia mitandao ya kijamii kwa usalama na kwa manufaa ili kuepuka athari zinazoweza kuhatarisha maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Wito huo umetolewa Oktoba 13, 2025, na wataalam wa Wizara hiyo walipoungana na wadau wa sekta ya umma na binafsi kutoa mafunzo ya usalama mtandaoni katika shule ya Sekondari ya Kilimani iliyopo mkoani Mwanza.

Wanafunzi walihimizwa kufikiri kwa makini kabla ya kuchapisha au kutuma taarifa mtandaoni ili kuepuka vitendo vya udanganyifu, unyanyasaji na uvunjaji wa maadili mtandaoni.

Aidha, walipewa elimu kuhusu umuhimu wa kuripoti matukio ya ukatili na unyanyasaji kupitia namba 116, utapeli mtandaoni kupitia namba 15040 au katika madawati maalum ya kuripoti matukio hayo.  

Mtaalam wa usalama mtandao na uchunguzi wa kidijitali, Bw. Yusuph Kileo, alieleza kuwa tafiti zinaonyesha watoto wengi hutumia simu bila uangalizi wa wazazi na hivyo kuwa katika hatari ya kukumbana na changamoto za kimtandao.

Alisisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao na kuhakikisha taarifa wanazoweka mtandaoni zina manufaa kwa sababu “mtandao hausahau.”

Katika mafunzo hayo, wanafunzi walifundishwa mbinu za kujilinda ikiwemo kutotoa taarifa binafsi kwa watu wasiojulikana, kuepuka tovuti zisizo salama na kutumia mitandao kwa maendeleo binafsi na ya jamii.