Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MAPINDUZI YA KIDIJITALI YANAYOENDELEA TANZANIA YAIVUTIA COMORO


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema Wizara inaendelea kuboresha sera na kuweka mikakati mbalimbali ili kuwezesha nchi kufikia mapinduzi ya kidijitali kutokana na kukua kwa teknolojia ikiwemo teknolojia zinazoibukia na akili mnemba (AI).  

Bw. Adulla ameyasema hayo tarehe 25 Novemba, 2024 ofisini kwake alipokuwa akizungumza na timu ya wataalamu wa TEHAMA kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Dijitali ya Comoro (ANADEN) iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Said Mouinou Ahamada waliombatana na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Said Yakoub  wakiwa katika ziara ya kujifunza hatua mbalimbali zilizofikiwa na pamoja na kutathmini maendeleo ya sekta ya mawasiliano na TEHAMA nchini.

“Natambua kuwa mnayo Wizara inayoshughulikia masuala ya TEHAMA lakini pia mna taasisi yenu inayoitwa ANADEN, ili kufikia mapinduzi ya kidijitali ni muhimu kuzingatia mambo matatu ya msingi ambayo ni kuwa na uendeshaji wa Serikali kidijitali na utoaji wa huduma kidijitali; kuiwezesha jamii kutumia huduma mbalimbali kidijitali na shughuli za uchumi kuendeshwa kidijitali”, amesema Abdulla.   

Bw. Abdulla amewataka wataalam kutoka nchini Comoro kuwa huru kujifunza kutoka katika Wizara hiyo na taasisi zake na iwapo watahitaji msaada wowote Wizara iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha hitaji hilo.

Wataalam hao wamepata nafasi ya kujifunza namna Tanzania inavyoendelea kupiga hatua katika mapinduzi ya kidijitali sambamba na kupitishwa kwenye taarifa za utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali na utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Huduma za Mtandao kutoka Comoro, Bw. Said Mouinou Ahamada, amesema tayari wanazo Kanuni za Usalama Mtandao, mkakati wa kitaifa wa kidijitali pamoja na sheria na sera kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi na kwamba wamekuja kujifunza ni namna ya kuweka mifumo ya Kidijitali katika serikali ili kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Wataalamu hao kutoka Wakala wa Maendeleo ya Huduma za Mtandao kutoka Comoro walifika nchini Tanzania kuanzia tarehe 21 Novemba, 2024 na kupata nafasi ya kutembelea, kujifunza na kubadilishana uzoefu na taasisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Wakala wa Serikali Mtandao (eGa) na Kituo cha Kuhifadhi Taarifa (NIDC).