Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MAGHALA MAKUBWA YA KUHIFADHI BIDHAA ZA BIASHARA MTANDAO KUJENGWA NCHINI.


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akiongoza kikao kazi kuhusu kupokea taarifa ya tathmini ya soko (market assesment) ya upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa maghala kuwezesha uhifadhi wa bidhaa za biashara mtandao tanzania tarehe 20 Februari, 2023, katika ukumbi Rafiki Hotel, jijini Dodoma.

Na Chedaiwe Msuya, WHMTH 

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imedhamiria kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya posta nchini kwa kujenga maghala ya kisasa ili kuwezesha uhifadhi wa bidhaa za biashara Mtandao na kuwasaidia wananchi kufikia masoko ya ndani ya nchi na nje ya nchi.

Akiongoza kikao cha kupokea taarifa ya tathimini ya soko na upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa maghala kuwezesha uhifadhi wa bidhaa za biashara mtandao Tanzania leo February 20 2023 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa lengo kubwa ni kuipeleka nchi kidijiti na kuleta maendeleo kwa watanzania.

"Leo tumefanya kikao kwa kushirikiana na wenzetu wa Oman kuhakikisha tunaibadilisha posta katika utendaji kazi wake ili kufikia soko kubwa zaidi likiwemo la nchi za Afrika Mashariki na SADC", amesema Dkt. Yonazi

Aidha, Dkt Yonazi amesema ujenzi wa maghala hayo ni kuhifadhi bidhaa za biashara Mtandao ili kuruhusu biashara mtandao kufikia masoko ya kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Mzee Suleiman Mndewa amesema kujengwa kwa maghala makubwa kutasaidia kupatikana kwa bidhaa kwa urahisi na kwa haraka.

"Ujenzi huu wa maghala utasaidia sana biashara mtandao kwa kuhifadhi bidhaa na kusaidia watanzania kuweza kupata bidhaa zenye ubora mahali popote walipo na kujenga uchumi wa nchi”, amesisitiza Dkt. Mndewa.

Naye Amina Mwantuya kutoka sekta ya uchukuzi amesema kuwa sekta hiyo ni wadau wa biashara mtandao katika kipengele cha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kupitia bandari, viwanja vya ndege na reli na tayari wanashirikiana na Wizara kupitia Sekta ya posta kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa unafanyika kwa kiwango cha kimataifa.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Constantine Kasese, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na uendeshaji wa Shirika la Posta Tanzania amesema kuwa lengo la Serikali ni kuendelea kuboresha sekta ya posta na biashara mtandao kwa kuboresha mazingira ya kuhifadhi na kusafirisha bidhaa zinazoharibika na zile zisizoharibika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kikao hicho kilikuwa cha kupokea taarifa ya  kamati iliyofanya tathmini ya soko na upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhi bidhaa za biashara mtandao nchini,  ambapo wadau kutoka sekta mbalimbali walijadili taarifa hiyo kwa lengo la kuboresha masoko ya biashara mtandao, uhifadhi wa bidhaa na usafirishaji.