Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MAENEO YOTE YALIYO KUWA BADO HAYAJAWEKWA ANWANI ZA MAKAZI YAKAMILIKE. DC UBUNGO


Na. Simon Kibarabara 

Serikali imeagiza kuwa maeneo yote yaliyokuwa na changamoto ya kuweka Namba za Nyumba na majina ya Mitaa yakamilishwe haraka ili zoezi hilo likamilike.

Hayo yamesemwa leo Juni 20, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Bw. Hashim Komba, wakati akifunga zoezi la Mafunzo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mtaa na Watendaji Kata pamoja na wakusanya taarifa wa zoezi hilo yaliyofanyika Ukumbi wa La Dariot, Ubungo Mkoani Dar es salaam.

Mhe. Komba amesisitiza kuwa washiriki wote wahakikishe wanatoa ushirikiano wa kufanikisha zoezi hili kwa kuwa ni zoezi la muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa letu.

“Hakuna atakayekwamisha zoezi hili kwa sababu ni zoezi la kitaifa kwa maendeleo ya taifa letu, tutatatua changamoto zote ili kusiwe na pakukwama katika zoezi hili” alisema Mhe. Komba
Akitoa salam kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa  Dar es salaam, Mhe. Komba amesema kazi ya serikali ni kutatua changamoto zote zinazotatiza zoezi hili ili kuwawezesha wataalam kufanya kazi yao ya uhakiki, usasishaji na kuweka maboresho sehemu zitakazohitaji kufanya hivyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo (DAS), Ndgu Hassan Mkwawa amesema Umoja na Ushirikiano katika kazi hii ndiyo siri ya kufanikisha kwa haraka na kwa ufanisi zoezi hilo la Uhakiki wa Anwani za Makazi.

Aidha, Ndgu Mkwawa aliwaeleza washiriki kuwa zoezi hilo litachukua muda wa wiki moja na nusu kukamilika, hivyo wakati wote wa utekelezaji kunahitajika utashi, utimamu na nidhamu ya hali ya juu.