Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MABADILIKO YA AKILI MNEMBA (AI) HAYAKWEPEKI - WAZIRI NAPE


Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema mabadiliko ya Akili Mnemba (AI) yana faida kubwa kwa nchi, na kwa sababu hiyo, Serikali imechukua hatua muhimu kwa kuandaa vyuo na kutoa elimu kuhusu teknolojia hiyo. 

Waziri Nape alieleza hili wakati akijibu swali kuhusu wasiwasi wa teknolojia hiyo kusababisha ukosefu wa ajira lililoulizwa na Mbunge wa Kawe, Mhe. Dkt Josephat Gwajima, Bungeni, jijini Dodoma leo Februari 09, 2024. 

Alisisitiza umuhimu wa kujiandaa na kukabiliana na mabadiliko haya kwa kuelimisha jamii na kutoa mafunzo kwa watoto.

“Tuliandae Taifa letu kwamba haya mabadiliko yana fursa ndani yake, ndio maana tunawafundisha watoto wetu, tunaifundisha jamii ili tusipitwe na teknolojia hiyo kwa sababu haya mapinduzi haya ya nne ya viwanda hayakwepeki na lazima tujiandae namna ya kuyakabili'." amesema Waziri Nape.

Aidha, alizungumzia mikakati ya kulinda watu na mabadiliko ya teknolojia hiyo, ikiwa ni pamoja na kuweka sheria, kanuni, sera, pamoja na kuwekeza katika mapinduzi ya TEHAMA. 

Mhe. Nape pia alimpongeza Rais kwa kuanzisha Wizara ya TEHAMA, ikionesha umuhimu wa kuwezesha mabadiliko haya katika nchi.