Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KUWENI WAZALENDO, TUMIKIENI TAIFA KWA KUACHA ALAMA - WAZIRI NAPE


Waziri wa Habari Mawasiliano, Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akizungumza wakati wa mkutano wake na wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo Aprili 30, 2022 jijini Dodoma.

 

 DODOMA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewataka wafanyakazi wa Wizara anayoisimamia kubadilisha utamaduni wa kufanyakazi kwa mazoea badala yake wawe wazalendo, wapendane na kila mfanyakazi kuhalalisha nafasi aliyonayo kwa kufanya kazi kwa kuacha alama

Waziri Nape ameyazungumza hayo wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa Wizara anayoisimamia kilichofanyika jijini Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa agizo lake alillolitoa wakati wa Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika mwezi Machi mwaka huu.

“Kila mmoja wetu ahalalishe uwepo wake katika nafasi yake, acheni kufanya kazi kwa mazoea, twendeni tukafanye kazi kwa kuacha alama, na kila mmoja wetu akiweka nia inawezekana na Wizara yetu itafanya vizuri zaidi”, Amezungumza Waziri Nape

Ameongeza kuwa Wizara hiyo ina jukumu kubwa la kuwatumikia wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuhakikisha inalipeleka Taifa sambamba na mabadiliko ya dunia katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na kuhabarisha na kuelimisha umma kidijitali

Kwa kuzingatia hilo, Waziri Nape amezitaka Idara zinazosimamia miradi ya Kitaifa inayotekelezwa chini ya Wizara hiyo kuhakikisha inawajengea uwezo watumishi wote kuhusu Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Mfumo wa Anwani za Makazi na Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili waifahamu miradi hiyo na kuwa mabalozi wazuri kwa wadau wa nje ya Wizara

Katika hatua nyingine, Waziri Nape amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kuona fahari kuitumikia Wizara hiyo na kila mmoja kumuona mwenzake ni zawadi kwake ili kwa pamoja wafurahie kazi wanazozifanya na mwisho wa siku wajivunie kuitumikia Wizara na kuacha alama

“Undugu ni kufaana, huku tunapokutana kwenye kazi ndio tunatengeneza familia, tusitafute fedha tukasahau utu na kuishi, tuheshimiane, tuhurumiane na tupendane, sisi kama viongozi wenu tutaendelea kusisitiza haki kwenye maeneo ya utawala”, amesisitiza Waziri huyo

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kwake ni wajibu na nia ya dhati kutengeneza mazingira bora ya utendaji kazi kwa watumishi wa Wizara hiyo ili wafanye kazi kwa furaha bila msongo wa mawazo na kuweza kutafakari vema na kuleta ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.