Habari
KONGAMANO LA C2C KUHARAKISHA UUNGANISHWAJI WA KIDIJITALI BARANI AFRIKA

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
Ongezeko la uunganishwaji na ujumuishwaji wa teknolojia ya kidijitali kunatengeneza fursa za ajira, kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji, na kunawezesha upatikanaji wa masoko ya kimataifa, hivyo kupunguza umasikini na ukosefu wa usawa.
Kongamano la connect to connect (C2C) limekuwa ni jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi kukutana, kubadilishana maarifa, na kuongeza thamani katika kuharakisha uunganishwaji wa kidijitali katika bara la Afrika.
Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla akifunga Kongamano la C2C leo tarehe 19 Septemba 2024 jijini Arusha.
“Wizara inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma katika enzi hii ya kidijitali kwa kuendelea kuziba pengo la kidijitali katika maeneo yote nchini kwa maendeleo endelevu”, amezungumza Bw. Abdulla.
Ameongeza kuwa, ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 inasisitiza kuwa teknolojia za kidijitali ni muhimu kwa kufanikisha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kwa sababu zinaboresha utawala bora, kuongeza utoaji wa huduma, na kuwawezesha wananchi kupitia upatikanaji wa taarifa na fursa.
“Serikali kupitia Wizara hii inajivunia kushirikiana tena na Kampuni ya Extensia Ltd ya Uingereza kufanikisha Kongamano hili kufanyika nchini ambalo limekuwa chachu ya kuharakisha ajenda ya uunganishwaji wa kidijitali”, amesisitiza Katibu Mkuu Abdulla.