Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KATIBU MKUU WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI AAGIZA JAMII NAMBA ITUMIKE KATIKA MIFUMO YOTE YA KUTOLEA HUDUMA


Na Chedaiwe Msuya, WHMTH, Da es Salaam.

Serikali imezitaka Taasisi za serikali kuhakikisha zinafuata miongozo na mifumo yote ya kutolea huduma za kidigitali nchini, kwa kutumia namba jamii ambayo ni namba yakitambulisho cha Taifa (NIDA).

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla, wakati akifunga kongamano la saba la TEHAMA 2023 Jijini Dar es Salaam  oktoba 20,2023 ambapo amesisitiza namba hiyo itumike na wananchi wanapotaka kutumia huduma anayoitaka ipatikane kwa urahisi.

"Taasisi mbalimbali za Serikali na za binafsi, hakikisheni mnafanya  tafiti na kutoa elimu kwa jamii kuhusu teknolojia bora ya akili bandia ambazo zitaleta tija ya kiuchumi kwa kutoa ajira kwa vijana na makundi maalum". Amesisitiza.

Aidha,katibu Mkuu huyo amesema serikali  imeendelea kuandaa mkakati wa uchumi wa kidigitali kwa kuboresha miongozo ya kisera na kisheria.

"Katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na miundombinu  itakayowezesha uwepo wa teknolojia  mpya na za kisasa zinazoibukia, serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha Miongozo ya kisera na kisheria". Amesema 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Mwasaga akisoma taarifa za utangulizi kuhusu mkutano huo, amesema lengo kubwa la kongamano hilo  ni kujenga uchumi wa kidigitali ambao ni jumuishi.