Habari
Katibu Mkuu wa Mawasiliano Aungana na Wadau wa TEHAMA katika Kongamano la 4 la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu EAC Kigali
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla ameungana na wadau mbalimbali wa masuala Teknolojia ya Habari na Ubunifu katika Kongamano la Nne la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community) lililofanyika katika Mji wa Kigali, nchini Rwanda.
Kongamano la Nne la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linalofanyika kuanzia tarehe 30 Machi, 2026 hadi 1 Aprili, 2026 katika Jiji la Kigali nchini Rwanda litaimarisha ushirikiano baina ya wadau ndani ya Jumuiya ya EAC huku likileta chachu ya kukuza uchumi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa nchi wanachama katika soko la kimataifa.
Kongamano hilo linaloongozwa na Kaulimbiu isemayo “Matumizi ya Akili Unde kwa ajili ya Afrika Mashariki yenye Ustahimilivu, Jumuishi na Ubunifu” liliwakutanisha viongozi wa ngazi za juu wa Serikali kutoka nchi wanachama wa EAC, wabunifu, wanataaluma na wadau wa maendeleo kujadili namna Akili Unde inavyoweza kusaidia sekta mbalimbali kuendana na mabadiliko ya Kiteknolojia Duniani.
Katika Kongamano hilo, Bw. Abdulla aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Aidha, Kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano kati ya sekta ya mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wadau wengine wa ubunifu katika kanda.
