Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KATIBU MKUU ABDULLA AZINDUA MAJARIBIO YA UTOAJI WA BARUA YA UTAMBULISHO KUPITIA MFUMO WA NaPA


Na. Mwandishi wetu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amezindua  majaribio ya kutoa huduma ya Barua ya Utambulisho wa Mkazi kupitia Mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi wa NaPA pamoja na vitendea kazi kwa watendaji wa Kata na Shehia zitakazofanyiwa majaribio kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Aprili 16, 2024 jijini Dodoma, Bw. Abdulla amesema kuwa mfumo wa Anwani za Makazi umetengenezwa kwa dhumuni la kuboresha utoaji wa huduma ndani ya Serikali na Sekta binafsi ili kuiwezesha nchi kunufaika na fursa za Uchumi wa kidijitali sambamba na kuimarisha masuala ya utambuzi na usalama ndani ya nchi.

Amesema kuwa Operesheni ya Anwani za Makazi ilikuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya Anwani za Makazi milioni 12.3 zilisajiliwa na taarifa zake kuhifadhiwa kwenye Mfumo wa Anwani za Makazi unaojulikana kwa jina la NaPA ambapo amesisitiza kuwa usalama wa eneo mtu anapoishi unaanzia kwa kutambua jirani yake ni nani. 

Hata hivyo kwa lugha rahisi, NaPA ni daftari la kidijitali la ukazi ambalo linawezesha Serikali Kuu, Serikali za Mtaa/Kata au Shehia pamoja na mambo mengine kujua idadi wa watu walio kwenye eneo husika na kuleta urahisi wa kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia uhalisia wa watu na huduma zilizopo katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Divisheni ya Uendelezaji Miji na Vijiji Bi. Rachel Kaduma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI amesisitiza kuwa zoezi la majaribio ya utekelezaji wa moduli ya utoaji wa barua ya utambulisho kidijitali kupitia mfumo wa NaPA litasimamiwa kikamilifu na OR-TAMISEMI kwa kiwango kikubwa kama inavyotarajiwa na kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wake ili matarajio ya serikali yaweze kufikiwa.

Vile vile, Bi.Kaduma ameeleza kuwa hatua hii ni utekelezaji wa zile R nne za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani Ile ya "Reforms" maana kupitia huduma hii tutakwenda kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma katika utoaji wa barua ya utambulisho pasipo kufika Ofisi za Ngazi za msingi.