Habari
KATIBU MKUU ABDULLA AONGOZA KIKAO CHA KAMATI TENDAJI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam.
Kamati tendaji ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla imefanya kikao cha kwanza kuhusu ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini.
Kikao hicho kilichofanyika Oktoba 8, 2024 katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam kimejadili na kuweka mikakati ya kushirikiana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika na unasaidia kuboresha huduma za mawasiliano na kuongeza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika maeneo ya vijijini.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya kamati hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Mawasiliano na Utangazaji wa Wizara hiyo, Mhandisi Nikusubila Mwambije, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini unalenga kujenga jumla ya minara 636 ambapo kati ya hiyo minara 621 ni minara ya simu na minara 15 ni ya Redio.
Ameongeza kuwa kupitia Mradi huo minara hiyo inakwenda kuongeza Mawasiliano ya simu na usikivu wa Redio ya Taifa kwa wananchi wengi walioko vijijini.
#MawasilianoNchiNzima #SmartTanzania