Habari
KARATU YALAZIMIKA KUONGEZA WATUMISHI WA HALMASHAURI KUFANIKISHA UHAKIKI WA TAARIFA ZA ANWANI ZA MAKAZI

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
Wakati zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi likiendelea katika Halmashauri sita (6) za Mkoa wa Arusha ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, halmashauri hiyo imelazimika kutoa watumishi 25 wa Kilimo na Maendeleo ya Jamii ili kufanikisha uhakiki huo.
Uhakiki huo endelevu, unaratibiwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI; Mkoa wa Arusha na Halmashauri za Mkoa wa Arusha.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Uhakiki wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Ndugu Innocent Jacob, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo mjini Karatu tarehe 18 Agosti, 2024.
Jacob amesema Halmashauri hiyo imelazimika kutoa watumishi wa kada nyingine kwa kuwa, watekelezaji wa zoezi hilo uwandani ni Watendaji wa Mitaa ama Vijiji, wakati kimuundo, katika mamlaka yoyote ya Mji Mdogo, hakuna vijiji wala mitaa bali kunakuwa na kata na vitongoji vinavyoongozwa na wenyeviti wa kuchaguliwa.
"Halmashauri ya Karatu ina jumla ya kata 14, kata 12 zina vijiji 68, na kila kijiji kina Mtendaji wake atakayetumika katika Uhakiki Uwandani. Kata mbili zilizosalia za Ganako na Karatu zinaunda Mamlaka ya Mji Mdogo wa Karatu, ambazo kimuundo zina jumla ya Vitongoji 25 tu", amesema Jacob.
Amesema kutokana na hali hiyo wamelazimika kutoa mafunzo upya kwa kada zilizoongezwa kusaidia kufanikisha Uhakiki huo tarehe 17 Agosti, 2024 na hivyo zoezi la Uhakiki limeanza rasmi tarehe 18 Agosti.
Akizungumza baada ya kufika Karatu, Mratibu wa Anwani za Makazi, kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Jampyon Mbugi amewataka watumishi hao wa Mji Mdogo wa Karatu, kuwa wadadisi na kuhakikisha wanaelewa vyema mafunzo, na hatimaye kutekeleza zoezi la uhakiki kwa tija na ufanisi.
Mhandisi Mbugi amewaeleza watumishi hao kuwa, wataalamu watakuwepo kutoa msaada wa kiufundi punde itakapohitajika ili kufanikisha uhakiki huo.
Aidha, mratibu huyo wa Anwani za Makazi kutoka wizarani aliwaeleza watumishi hao kuwa, Serikali inawekeza kwa watumishi, utaalamu wa utekelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi ili kuimarisha uendelezaji wa Mfumo kwani hata wakihamishwa kituo cha kazi wataendelea kutumika katika maeneo watakakohamia.