Habari
Kamati ya Uongozi ya Usimamizi wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Intaneti ya Kasi Yafanya Kikao cha Kwanza Dodoma
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Usimamizi wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Intaneti ya Kasi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, ameongoza kikao cha Kwanza cha kamati hiyo kilichofanyika leo, Juni 25, 2026, katika Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba, alisema kikao hicho ni hatua muhimu katika kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huduma za intaneti ya kasi bila kujali maeneo wanayoishi.
Mhandisi Magomba alisema kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi sasa asilimia 94 ya Watanzania wamefikiwa na huduma za intaneti ya kasi, huku asilimia 35 wakifikia huduma za teknolojia ya kizazi cha tano (5G). Alieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 wananchi wote nchini wanapata huduma za intaneti ya kasi kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, alisisitiza kuwa matumizi ya intaneti yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuwezesha malipo ya kidijitali, kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali na kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku, hususan kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA na ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati, Dkt. Nkundwe Moses, Mwasaga alisema kamati hiyo ina jukumu la kuangalia namna matumizi ya intaneti ya kasi yanavyoweza kuimarisha uchumi wa kidijitali nchini kupitia uandaaji wa mikakati, sera na miongozo inayoweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania.
Dkt. Nkundwe aliongeza kuwa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Intaneti ya Kasi utasaidia kuongeza ushindani wa uchumi wa kidijitali wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa. Alisema mkakati huo pia utachangia kufikiwa kwa azma ya taifa ya kujenga uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2030.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote kupitia kamati hiyo jumuishi ni muhimu katika kuonesha mchango wa TEHAMA katika kukuza Pato la Taifa, kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
