Habari
KAMATI YA UFUNDI YAJADILI HATUA ZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAGHALA YA KISASA YA BIASHARA MTANDAO.
Na Mwandishi wetu-WMTH Dodoma
Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Ujenzi wa Maghala ya Kisasa ya Kuhifadhi, Kusafirisha na Kusambaza Bidhaa ili kuwezesha Biashara Mtandao imekutana leo tarehe 23 Juni 2026 jijini Dodoma kujadili hatua za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaolenga kuimarisha biashara mtandao nchini.

Akifungua na kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Huduma za Posta kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Bi. Caroline Kanuti amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kufanikisha utekelezaji wa mradi wa Multi-modal Logistics Business Park (MMLBP) utakaoongeza uwezo wa Tanzania kuwa kitovu cha biashara mtandao katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara Mtandao, Fedha na Uwakala, Bw. John Mwakalonge, aliwasilisha taarifa ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo pamoja na mapendekezo mbalimbali yatakayowezesha kuendelea kwa utekelezaji wake kwa ufanisi zaidi.
Washiriki wa kikao hicho ambao ni wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali na wadau walipata fursa ya kuchangia maoni, kujadili changamoto zilizobainishwa na kupendekeza mikakati ya kuboresha utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa wakati na kufikia malengo yaliyokusudiwa huku ukichochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini Tanzania.
