Habari
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA WIZARA YA HABARI KWA KUONGEZA MAKUSANYO KUPITIA TAASISI ZAKE

Na Isabella Katondo, WHMTH, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa usimamizi mzuri wa Taasisi zilizo chini yake ambazo zimeweza kuvuka malengo katika ukusanyaji wa mapato.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 22, 2024 baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kupokea taarifa ya utekelezaji wa mipango na bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 na makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2024/25 iliyowasilishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb).
Akitoa salamu hizo za pongezi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Ally Jumbe Mlaghila (Mb) alimpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uongozi wake makini na ubunifu wake wa kutafuta fedha na kujituma.
“Tunataka kupeleka pongezi nyingi sana kwa TCRA, pamoja na kukusanya mapato lakini tunawapa pongezi kwa kazi kubwa mnayofanya ya usalama wa kidijitali na usalama wa anga letu la kidijitali. TCRA mmehakikisha pesa zetu na pesa za watanzania lakini pia mambo yenu mengi yako salama” alisema Mhe. Mlaghila.
Kamati pia imeielekeza Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuhakikisha inasimamia umaliziaji wa minara 758 ili ikamilike kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.