Habari
KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YATAKA WABUNIFU WA TEHAMA KULINDWA

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuandaa sera na sheria zitakazowalinda wabunifu wa TEHAMA, ikizingatiwa kuwa kumekuwa na changamoto za wabunifu wengi kushindwa kufanikisha bunifu zao au hata kuzuiliwa kuziendeleza.
Ushauri huo umetolewa na kamati hiyo wakati wa ziara katika ofisi za Tume ya TEHAMA (ICTC), tarehe 16 Machi 2025, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutembelea shughuli za taasisi hiyo, ikiwemo mradi wa ujenzi wa kituo cha Ubunifu cha TEHAMA kilichopo katika mtaa wa Upanga.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb) aliipongeza Serikali kwa hatua ya ujenzi wa kituo hicho pamoja na uanzishaji wa vituo nane vingine vya ubunifu wa TEHAMA vinavyoendelea kujengwa katika miji mbalimbali.
Sambamba na hilo, Kamati imepongeza mpango wa Serikali wa kuanzisha kwa Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Nala jijini Dodoma, ambacho kitatoa fursa kwa vijana wengi kupata mafunzo bila kujali kiwango chao cha elimu au kuwa na vyeti rasmi.
Mhe. Kakoso aliongeza kuwa Tanzania inalenga kuwa jamii isiyotegemea fedha taslimu (cashless society), hivyo kuna uhitaji wa kuwa na wabunifu na wataalam wengi wa TEHAMA watakaobuni na kutengeneza mifumo ya kidijitali inayohitajika.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) alisisitiza kuwa Wizara inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha bunifu za vijana zinakuwa na tija.
“Vijana wengi wa Tanzania ni wabunifu na wamekuwa wakitengeneza bunifu mbalimbali, lakini wamekuwa wakifanya kazi kiholela. Sasa tunakwenda kurasimisha bunifu zao ili ziwe halali na ziwe na manufaa,” alisema Naibu Waziri Mahundi.
Ameongeza kuwa, Kituo Kikuu cha Ubunifu cha Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU – International Telecommunication Union), kilichopo jijini Dar es Salaam, ni moja kati ya vituo 17 duniani vilivyoanzishwa kwa lengo la kukuza na kuunganisha wabunifu wa kidijitali duniani kote.
Akiwasilisha taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga, alisema kuwa Tume hiyo inaendelea kutekeleza ujenzi wa Kituo Kikuu cha Ubunifu cha TEHAMA jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuchochea mabadiliko ya kidijitali na kuendeleza ubunifu, ujasiriamali, na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.