Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU IMEITAKA SERIKALI KUHAKIKISHA TAASISI ZINALIPWA MADENI YAO YA MUDA MREFU


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka serikali kuhakikisha taasisi zilizochini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zinalipwa madeni yao ya muda mrefu ili ziweze kujisimamia na kujiendesha kibiashara.


Akizungumza  Dar es Salaam  jana, baada ya kuitembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso alizitaja taasisi zilizotajwa kuwa na madeni ya muda mrefu na kushindwa kukopesheka ni Shirika la Posta, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Alisema kuwa ni lazima serikali kuhakikisha inasimamia madeni hayo ili mashirika hayo yaweze kukopesheka na kujiendesha kibiashara.

Kakoso alisema TTCL, Posta, TSN na TBC zina miradi mingi lakini kutokana na madeni makubwa haziwezi kukopesheka na kujiendesha hivyo, waweke mikakati ya kuwasaidia.
Pia alishauri serikali ihakikishe mkongo wa taifa unaosimamiwa na TTCL unajiendesha  kibiashara ili kuleta mapinduzi katika sekta ya mawasiliano.


"Wizara iangalie namna ya kuongeza bajeti kwa TBC kwani kutokana na bajeti yao haiwezi kwenda kwenye ushindani wa soko la habari lakini katika Chaneli ya Safari haipati chochote na ndio maana wanarudia vipindi kwa sababu hawana uwezo wa kuandaa vipindi vipya kwa kuwa hawana fedha, muone namna ya kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii," alisema Kakoso.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema kuwa mpango wao ni  kuhakikisha madeni yote yanalipwa kwani TSN pekee inadai zaidi ya Sh bilioni 11, na tayari wameanza uhakiki wa madeni yanayoweza kulipwa  yalipwe na yanayoweza kugeuzwa kuwa mtaji wafanye hivyo.

Nape alisema  mchakato wa kuzifanya taasisi hizo kujiendesha kibiashara unaendelea na ndio maana wamewapa TTCL  mkongo na kituo cha data wasimamie na kujiendesha.

Pia alisema  wamefanya mabadiliko ya sheria ya posta ili kuwafanya waweze kujiendesha kibiashara sambamba na 
kuwataka kuwa na ubia na taasisi mbalimbali.

"Tumepokea maelekezo ya kamati ya bunge ya kuharakisha mchakato wa taasisi hizo zijisimamie kibiashara. Kuhusu upatikanaji wa huduma za redio mipakani, tumeelekeza TTCL kushirikiana na watoa huduma za redio kuongeza kasi ya upatikanaji wa masafa ya ndani," alieleza Nape.

Pia alielekeza TTCL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuweka miundombinu ya mkongo wa taifa kwenye nguzo za za umeme badala ya kufukia ardhini jambo ambalo linaongeza usalama.