Habari
KAMATI TENDAJI YA MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI YAJADILI UTEKELEZAJI NA MPANGO KAZI WA 2025/26

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, ameongoza Kikao cha Saba cha Kamati hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara, Mji wa Serikali – Mtumba, Dodoma.
Bw. Abdulla aliongoza kikao hicho leo tarehe 18 Agosti, 2025 akiwa sambamba na Mwenyekiti Mwenza, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi.
Katika kikao hicho, wajumbe walipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, sambamba na kuupokea mpango kazi wa utekelezaji wa mradi kwa mwaka wa fedha 2025/26 uliowasilishwa na Wataalam wa Kamati ya Watalaamu ya mradi huo.
Wajumbe wa Kamati Kuu Tendaji ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), waalikwa pamoja na Sekretarieti wakifuatulia mawasilisho katika Kikao cha Saba cha Kamati hiyo kilichofanyika leo, Agosti 18, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mji wa Serikali – Mtumba, Dodoma.
Aidha, kikao hicho kiliangazia maendeleo yaliyopatikana hadi sasa kupitia mradi huo na kutoa mapendekezo ya maboresho kwa lengo la kuhakikisha azma ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali na kukuza uchumi wa kidijitali nchini inafanikiwa.
Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ni mradi unaoratibiwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia unaolenga kuongeza ufanisi wa Serikali katika utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia TEHAMA, kuimarisha uwajibikaji na kuchochea ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya taifa.