Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Kairuki Aagiza Ujenzi wa Shule ya Msingi Mlembule ukamilike ifikapo Julai 30.


Na Mwandishi Wetu, Mpwapwa - Dodoma


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha ujenzi wa Shule Mpya ya Awali na Msingi Mlembule unakamilika ifikapo Julai 30, 2026 kama ilivyopangwa, huku akisisitiza kuwa ubora wa kazi usiathiriwe kwa sababu ya kukimbizana na muda.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika Kijiji cha Mlembule, Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Kairuki alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuongeza fursa ya kupata elimu ya msingi yenye ubora.

Alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia Programu ya Boosting Primary Student Learning (BOOST) kwa gharama ya Shilingi 302,200,000. Hadi sasa, Shilingi 269,642,506.40 zimetumika, huku Shilingi 32,557,493.60 zikiwa zimesalia kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki. Mradi huo ulianza Februari 15, 2026 na kwa sasa umefikia hatua ya umaliziaji.

Waziri Kairuki pia alielekeza kuwa fedha zilizobaki zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na taarifa za matumizi yake ziwasilishwe kwa uwazi. Aidha, aliipongeza Halmashauri kwa kutumia mfumo wa Force Account katika utekelezaji wa mradi na kutangaza zabuni kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi (NeST), akisema hatua hiyo imeongeza uwazi, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya fedha za umma.

Ili kuhakikisha shule inaanza kutumika mara moja baada ya kukamilika, Waziri Kairuki alizitaka mamlaka husika kuanza mapema maandalizi ya samani, madawati, huduma za maji safi, umeme na walimu wa kutosha. Pia alisisitiza shule hiyo iunganishwe na huduma za TEHAMA ili wanafunzi wanufaike na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia.

Waziri Kairuki alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuelekeza fedha nyingi katika miradi ya elimu, sambamba na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2024 inayolenga kujenga ujuzi, maarifa na uwezo wa wanafunzi kujiajiri na kuajiriwa.

Akihitimisha ziara hiyo, Waziri Kairuki aliwataka wazazi na wananchi wa Kijiji cha Mlembule kulinda miundombinu ya shule hiyo na kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kuanza shule wanaandikishwa na kuhudhuria masomo. Alisema ushirikiano wa jamii katika kutunza miradi ya maendeleo ni muhimu ili uwekezaji wa Serikali uendelee kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.