Habari
KAIRUKI: FAIBA IFIKIKE, IWE YA UHAKIKA NA NAFUU KWA WANANCHI.
Na Mwandishi Wetu- WMTH, Dar es salaam.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (mb) amelitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza kasi ya upanuzi wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) kwa kuhakikisha mtandao unaowafikia wananchi unaambatana na gharama nafuu, huduma ya uhakika na huduma bora kwa wateja.
Ameeleza hayo wakati akizindua Awamu ya Pili ya Mradi wa FTTH tarehe 21 Agosti, 2026 huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya nyumba zilizofikiwa pekee, bali kwa idadi ya wananchi wanaounganishwa na kunufaika na huduma hiyo.
Aidha, Waziri Kairuki ameitaka TTCL kupanua huduma katika makazi, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali, kwa kurahisisha usajili, kupunguza muda wa kuunganisha wateja na kuimarisha ubora wa mtandao na utatuzi wa haraka wa malalamiko ya wateja.
"Vipimo vya utekelezaji vizingatie wateja waliounganishwa, muda wa kuunganisha, kasi halisi, upatikanaji wa huduma, utatuzi wa malalamiko, kuridhika kwa wateja na mapato ya uwekezaji," amesema Waziri Kairuki.
Amesisitiza kuwa intaneti ya kasi si anasa bali ni nyenzo ya uzalishaji, maarifa na kuongeza kipato, akiwataka wananchi, wafanyabiashara, vijana na wanafunzi kuitumia kupata elimu, masoko, huduma za Serikali na fursa za uchumi wa kidijitali. Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga angalau asilimia 70 ya wananchi kutumia TEHAMA na zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali kupatikana kidijitali ifikapo mwaka 2050.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo mwaka iliyoishia Juni 2026 zinaonesha kuwa usajili wa intaneti umefikia 62,793,986, matumizi ya data yamefikia Petabaiti 1,041, lakini usajili wa Faiba Nyumbani ni 178,904 pekee. Awamu ya Kwanza ya FTTH imefikia home passes 280,000, huku Awamu ya Pili ikilenga kuongeza home passes 400,000.
Waziri amehitimisha kwa kutaka Awamu ya Pili iwe ya kasi zaidi, wateja wengi zaidi, huduma bora na vifurushi nafuu, huku akiwataka wananchi kulinda miundombinu ya mawasiliano dhidi ya wizi na uharibifu.
