Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

JUKWAA LA WAHARIRI (TEF) WAMPA WAZIRI NAPE TUZO YA KIHISTORIA


 

Jukwa la Wahariri Tanzania limempa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye Tuzo kwa Mchango wake mkubwa na ushirikiano na Wahariri na Vyombo Vya habari nchini.

“Sisi kama Wahariri tumefanya kazi na mawaziri wengi kwa nyakati tofauti. Hatujawahi kuwaza kumpa tuzo waziri yeyote tuliyefanya naye kazi, zaidi ya kwamba baadhi tuliishia kuwafungia habari zao zisichapishwe kwenye vyombo vyetu kutokana na utendaji wao dhidi ya vyombo vy ahabari, kwani badala ya kuwa walezi wa taaluma, waligeuka washindani wa taaluma” amesema Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri nchini Bwana Deodatus Balile wakati wa kutoa tuzo hiyo kwa Mhe. Nape.

Balile ameongeza kuwa katika historia ya kuanzisha kwa Jukwaa hilo, hali imekuwa tofauti kwa Mhe. Nape kwa vipindi vyote viwili alivyoongoza wizara yenye dhamana na masuala ya habari kwani amejihusisha kikamilifu na vyombo vya habari. 

“Umeshiriki mikutano yetu, mijadala, makongamano, uchunguzi kwa wavamizi wa vyombo vya habari na wakati mwingine, mikutano ya ana kwa ana na viongozi wetu wa wahariri au waandishi mmoja mmoja aliongeza Balile.

Balile katika Hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Kikao Cha Kitaaluma Cha 12 Cha Jukwaa la Wahariri Tanzania ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia UHURU wa Vyombo Vya Habari kwa kufungulia Vyombo vilivyokuwa vimefungiwa.

Akipokea tuzo hiyo, Mhe. Nape amewashukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania kwa kumpatia Tuzo hiyo na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae ndio amekuwa anamuelekeza kutekeleza yote yaliyofanyika katika muda wa uongozi wake. 

“Yote niliyoyafanya ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mimi nimetekeleza yote kama nilivyoelekezwa” amesema Mhe. Nape Nnauye.

Jukwa la Wahariri limempa Mhe. Nape tuzo hiyo maalum ambayo ni ya kwanza na ya aina yake kutolewa na Wahariri kwa Waziri yeyote hapa nchini tangu kuanzishwa kwa Jukwaa hilo