Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

IRINGA WAANZA ZOEZI LA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI KIDIJITALI.


*Viongozi na Wananchi Waaswa Kushirikiana.

Na Mwandishi wetu - WMTH, Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Benjamin Sitta, ametoa rai kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji kuwasaidia wananchi kutatua changamoto zote za majina ya barabara na kuhakikisha wanapewa nafasi ya kupendekeza majina ya barabara na mitaa yao.

Mhe. Sitta ametoa rai hiyo leo wakati akifungua zoezi la uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi kidijitali katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Katika hotuba yake, Mhe. Sitta amewataka viongozi na wananchi kushirikiana ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi ili mfumo huo uwe na taarifa sahihi zitakazochochea maendeleo endelevu katika Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Naye Bw. Bakari Mwamgugu, Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema kupitia Mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi (NaPA) wananchi wanapata huduma ya barua za utambulisho kidijitali, hadi kufikia Septemba 21, 2025 jumla ya barua za utambulisho 668,558 zimetolewa nchi nzima, huku Manispaa ya Iringa barua 6,925 zilitolewa.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Mashaka Makuka amesema TAMISEMI ni wanufaika wakubwa wa mfumo wa Anwani ya Makazi kwa kuwa unawezesha upatikanaji wa taarifa muhimu na kusaidia kupunguza gharama za utekelezaji ndani ya Serikali.