Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Huduma za Mawasiliano Zaimarika Ndani ya Siku 100 za Rais Samia


Na Mwandishi Wetu, WMTH-Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma

 

Katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kukua kwa kasi ikichangiwa na uwekezaji ulioendelea kufanywa na Serikali hususan kwenye ujenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano ikiwemo Minara ya Mawasiliano na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

 

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), wakati akiwasilisha taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais Samia za mafanikio ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita (Muhula wa Pili), katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, tarehe 04 Februari, 2026.

 

Akitoa Takwimu za ukuaji huo mbele ya Waandishi wa Habari, Waziri Kairuki amesema kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 99.3 Oktoba, 2025 hadi laini milioni 106.9 Januari, 2026 sawa na ongezeko la asilimia 7.7. Watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 56.3 Oktoba, 2025 hadi milioni 58.1 Januari, 2026 sawa na ongezeko la asilimia 3.2. Na Watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao wa simu wameongezeka kutoka milioni 71.7 Oktoba, 2025 hadi Milioni 76.5 Januari, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 6.7.

 

Kwa upande wa gharama za Mawasiliano, Waziri Kairuki alieleza kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kudhibiti ongezeko la gharama za Mawasiliano ambapo gharama za kupiga simu ndani ya Nchi zimeendelea kuwa Shilingi 29 kwa dakika. Aidha, wastani wa bei ya Data bila kifurushi nayo imeendelea kubaki Shilingi 9.35 kwa kila MB 1 hadi.

Kupitia Takwimu inaashiria kuwa, Serikalo inaendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za mawasiliano. Hatua ambayo inapelekea wananchi kufikiwa na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kidijitali kama vile huduma za Kifedha, afya, kwa urahisi na kwa haraka.

 

Vilevile, Waziri Kairuki aliongeza kuwa ongezeko la huduma za Mawasiliano limechochea ukuaji wa uchumi wa watu na Taifa kwa ujumla hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imejikita katika kujenga uchumi wa kidijitali.

 

 

#KaziNaUtu

#TunasongaMbele

#TabasamuLaUtu

#Siku100zaRaisSamia