Habari
Heshima ya maafisa habari tutaendelea kuisimamia, timizeni wajibu wenu - Mhe. Nape

Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amewataka Maafisa Habari wa Serikali kutimiza wajibu wao katika kuisemea Serikali hasa kwenye shughuli za maendeleo zinazotekelezwa kwenye maeneo yao ya kazi.
Hayo ameyasema leo Ijumaa tarehe 21 Juni, 2024 akifunga kikao kazi cha 19 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 21 Juni, 2024.
“Heshima ya Maafisa Habari kwenye nchi yetu nawaahidi kuendelea kuisimamia nanyi timizeni wajibu wenu. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mambo mengi sana, katangazeni shughuli zote zinazotekelezwa na Serikali kwa tafsiri sahihi wananchi wetu wapate kuelewa na kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo ya nchi yetu.”
“Kazi yetu ni kubwa sana ya kuwa katikati ya Serikali, Taaasisi zetu na Umma tunaouhudumia. Tunawajibu mkubwa sana kwa taasisi zetu na serikali kujua yanayoendelea kwa umma. Pamoja na kupeleka taasisi kwa umma pia tuwe ni maafisa habari wa kutoa taarifa kwa umma na kuzipeleka kwenye taasisi zetu ili kuimarisha utendaji kazi wetu.”
Kikao kazi hicho cha 19 cha Maafisa Habari, mawasiliano na uhusiano wa serikali ni moja ya njia ya maafisa hao kujifanyia tathmini ya utendaji kazi wao wa kila mwaka kwa kuwa wao ndiyo wenye jukumu la kuimarisha mawasiliano kati ya wananchi na serikali yao kwa kuwaeleza “Heshima ya maafisa habari naendelea kuisimamia, timizeni wajibu wenu” - Mhe. Nape.
=MWISHO=