Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

HAKIKISHENI MNAPATA NAMBA YA NIDA (JAMII NAMBA): WAZIRI MKUU MAJALIWA


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Saalam

Serikali imesema ili kuhakikisha mkakati wa uchumi wa kidijitali unatekelezwa kwa tija, itaweka mkazo kuhusu umuhimu wa namba ya NIDA ambayo ni namba pekee itakayomtambulisha kila raia nchini.

Namba ya NIDA ndio Jamii namba itamwezesha mwananchi kupata huduma za kijamii na kiuchumi kutoka Serikalini na sekta binafsi na hivyo ni muhimu kwa kila Mtanzania kuwa na namba hiyo.

Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa tarehe 17 Oktoba, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifunga Kongamano la Nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Serikali imeelekeza kuwa namba ya NIDA ndiyo namba jamii itakayotumika katika utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali hapa nchini. Kwa msingi huo, niwahimize Watanzania wenzangu kuhakikisha wanapata namba ya NIDA ambayo ndiyo namba jamii,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza;

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mmoja anatumika na kutambuliwa, pamoja na kuzitambua sekta rasmi, kama njia ya kufikia mapinduzi ya kidijitali katika nyanja mbalimbali na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Kwa njia hiyo, watu wataweza kulipa kupitia namba ya NIDA badala ya kutumia fedha taslimu, hivyo kuongeza usalama katika fedha.”

Waziri Mkuu alisema namba hiyo itasababisha mifumo kusomana, na kufanya iwe rahisi kupata huduma mahali popote, ikiwemo kununua tiketi, huduma za kifedha, na ununuzi wa bidhaa.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaelekeza viongozi wa taasisi zote za Serikali na zisizo za kiserikali, kuhakikisha mifumo yao inasomana ili kubadilishana taarifa kwa urahisi.

“Serikali inaendelea na mfumo wa Jamii X-Change, hivyo ni muhimu kuhakikisha utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Samia (Rais wa Jmhuru ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan) ya mifumo kusomana unakamilika kama ilivyopangwa,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

“Wizara hakikisheni mnasimamia mifumo yote inasomane ndani ya taasisi za serikali na nje ya taasisi za sekta binafsi, kwani kufanya hivyo kutarahisisha mawasiliano kati ya taasisi hizo, zikiwemo za kifedha,” aliongeza.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu Majaliwa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), alisema Wizara yake inaendelea kuratibu ujenzi wa mifumo mbalimbali ukiwemo wa Anwani za Makazi (NaPA), unaowezesha utambuzi wa makazi, biashara na maeneo ya huduma za kijamii.

Alitolea mfano wa namna mfumo huo ulivyosaidia utambuzi wa wananchi na makazi yao wakati wa majanga ya maporomoko ya udongo yaliyotokea Hanang na mafuriko katika Wilaya ya Kibiti.

Waziri Silaa alisema pia Mfumo huo wa Anwani za Makazi upo katika hatua ya majaribio ya utolewaji wa barua ya utambulisho kidijitali ukitarajiwa pia kutumika kutangaza vivutio vya utalii.

Alibainisha kwamba wizara inaendelea kuratibu ujenzi wa mifumo ya Jamii Namba, Jamii X-Change, na Jamii Portal, kwa kuwa ni mifumo muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidijitali, na itasaidia katika utambuzi na ubadilishanaji wa taarifa.