Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YA TANZANIA YASAINI HATI YA MASHIRIKIANO NA KOREA KUSINI KUHUSU MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI


Na Innocent Mungy

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia makubaliano na kusaini wa hati ya ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Korea kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi unaondelea kutekelezwa nchini. Tukio hili muhimu lilifanyika nchini Korea Kusini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Bw. Mohammed Khamis Abdulla, alisaini hati hiyo ya makubaliano ya ushirikiano kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Dkt. KO Kidong, Makamu wa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama (WMDU), akisaini kwa niaba ya Jamhuri ya Korea jijini Seol mnamo tarehe 9 Novemba 2023.

Lengo la makubaliano haya ni kushirikiana katika utekelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi nchini Tanzania. Ushirikiano huu wa miaka mitano utajumuisha kubadilishana ujuzi na uzoefu, kuboresha mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi unaojulikana kama NaPA, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani, pamoja na kuhamasisha na kutoa elimu kwa umma kuhusu suala la Anwani za Makazi nchini Tanzania.

Hatua hii inalenga kuimarisha Mfumo wa Anwani za Makazi nchini Tanzania ili kuchochea maendeleo kwenye sekta zote za uchumi zinazotegemea mfumo wa Anwani na makazi.  Aidha, Ushirikiano huu utasaidia kuwezesha mawasiliano rahisi na upatikanaji bora wa huduma kwa wananchi kupitia Anwani za Makazi hivyo kuchochea maendeleo kwa jamii.