Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DOLA BILIONI 4.7 ZA MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI KUENDELEZA WATAALAMU WA TEHAMA


Na Faraja Mpina, WHMTH, Dodoma.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali imetenga kiasi cha dola za kimarekani bilioni 4.7 kwa ajili ya kuwezesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wataalamu wa TEHAMA nchini.

Takwimu hiyo imetolewa leo Septemba 9 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla katika hafla ya kuwakabidhi vyeti vya ufadhili wa masomo ya muda mrefu nje ya nchi watumishi wa umma wapatao 20 kutoka katika Wizara, taasisi za umma na halmashauri za miji na wilaya.

Katibu Mkuu Abdulla amesema watumishi hao 20 wamepatikana baada ya kuchakata maombi 211 ya watumishi wa kada ya TEHAMA walioomba kupatiwa ufadhili wa masomo ya muda mrefu nje ya nchi.

“Nitoe rai kwa kila aliyepata ufadhili huu, kutumia kikamilifu fursa hii kujifunza kwa bidii kwa lengo la kuongeza uelewa na maarifa ili mtakaporudi muweze kuleta mabadiliko chanya yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za Serikali”, amezungumza Abdulla. 

Amesema kuwa juhudi hizo zinazofanywa na Serikali zinapaswa kuwa chachu kwa sekta Binafsi kuungana na Serikali kuongeza vyanzo vya ufadhili na kufanya uwekezaji wa kukuza rasilimali ya wataalamu wa TEHAMA nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema kuwa watumishi hao wanakwenda kuongeza ujuzi na maarifa na watakaporejea ofisi hiyo itahakikisha wanatumika vizuri kitaifa na kimataifa.

Naye Bw. Gerald Mbwafu, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatambulika katika balozi za Tanzania lakini pia kuwa wazalendo na kuiwakilisha nchi vizuri.

Awali Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya, Bi. Salome Kessy akitoa taarifa ya ufadhili huo amesema Mradi wa Tanzania ya kidijitali umepanga kutoa ufadhili wa mafunzo kwa watumishi 500 kati ya hao watumishi 50 watapatiwa mafunzo ya muda mrefu na watumishi 450 watapatiwa mafunzo ya muda mfupi katika maeneo ya teknolojia zinazoibukia.

 Aidha ameanisha watumishi 20 waliotunukiwa vyeti vya ufadhili kwa awamu ya kwanza ni kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (2), Ofisi ya Rais Menejuimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (1), Mamlaka ya Serikali Mtandao (2), OR-TAMISEMI (3), Wizara ya Fedha (2), NIDC (3), TTCL (3), NIDA (1), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (2) na Chuo Kikuu Huria (Open University) (1).