Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. NDUGULILE ASEMA ANATAKA KUONA MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE MPYA


  • Ataka Teknolojia rahisi zitumike kufikisha huduma za mawasiliano
  • Asema Maboresho ya Sheria, Kanuni Yafanyike Kuendana na Mabadiliko ya Teknolojia
  • Tafiti Zifanyike Kubaini Mchango wa TEHAMA katika Ukuaji wa Uchumi

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema anataka kuona Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mpya inayoendana na Wizara mpya wakati wa ziara yake alipotembelea taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara yake na kufanya kikao na wajumbe wa bodi, menejimenti na wafanyakazi ili kufahamiana na kuwa na uelewa wa pamoja kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa makujumu ya Wizara hiyo mpya ili kuakisia maono na ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuunda Wizara hiyo mwezi Desemba, 2020

 

Dkt. Ndugulile amesema kuwa hivi sasa UCSAF inatumia shilingi milioni 350 kujenga mnara mmoja wa mawasiliano kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara, mbuga za wanyama, misitu na mipakani ambapo amesema gharama hiyo ni kubwa hivyo ameitaka UCSAF kubuni teknolojia rahisi zitakazotumika kuongeza wigo wa kufikisha huduma za mawasiliano nchini kwa gharama nafuu

 

Pia, ameongeza kuwa Wizara ishirikiane na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kufanya utafiti ili kubaini mchango wa TEHAMA katika ukuaji wa uchumi kwa kuwa taarifa iliyopo sasa ni kuwa TEHAMA inachangia pato la taifa kwa asilimia 0.5 wakati taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi TEHAMA na huduma za mawasiliano kwa kiasi kikubwa

 

Amesema kuwa Wizara ikamilishe uandaaji wa sheria ya TEHAMA na kuboresha sheria zilizopo za taasisi za Wizara hiyo pamoja na kanuni ili ziweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani ili TEHAMA iweze kufanikisha zaidi ukusanyaji wa mapato na kuwekeza zaidi kwenye TEHAMA kwa kuwa ukiongeza asilimia 1% ya uwekezaji kwenye TEHAMA inachangia pato la taifa kwa asilimia 10%

 

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema kuwa wameambatana na Dkt. Ndugulile kwenye ziara hiyo ili kutengeneza dira ya pamoja ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kidijitali. Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa hadi sasa wamefikisha huduma za mawasiliano kwenye vijiji 3,119 vilivyopo kwenye kata 994 zenye wakazi 12,241,492 na amekiri kufanyia kazi maelekezo ya Waziri huyo ili wananchi wengi zaidi wapate huduma za mawasiliano

 

Naye Afisa Mhasibu Mkuu wa UCSAF, Josephine Mtei amesema kuwa ziara ya Waziri huyo na viongozi wa Wizara ni jicho la taasisi yao la kuona utendaji wao na wako tayari kushirikiana na Wizara kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi wengi zaidi ili kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020- 2025