Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. CHAULA APOKEA UGENI KUTOKA SHIRIKA LA POSTA KENYA


DAR ES SALAAM

*Azipongeza Posta Tanzania na Posta Kenya kufungua milango ya biashara

 *Asisitiza kukuza lugha ya kiswahili

 *Posta yatarajia ugeni kutoka  Kongo Brazzaville na Zimbabwe           

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amepongeza Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Kenya kwa kuendelea kuimarisha mahusiano yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Hayo ameyasema leo wakati alipopokea ujumbe kutoka Shirika la Posta Kenya ulioongozwa na Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Bw. Dan Kagwe aliyeambatana na Milka Mugwe, Meneja Uendeshaji na Huduma kwa Wateja pamoja na Joel Mageto,Meneja wa Miradi Maalum na Katibu katika Ofisi ya Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam.

Dkt Chaula ameeleza kuwa kuwepo kwa mahusiano mazuri na ushirikiano wa moja kwa moja kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Kenya ni chachu ya kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Dkt Chaula ameeleza kuwa ni vizuri kuboresha matumizi ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano na kulinda utaifa na heshima ya nchi zetu.

"Ushirikiano huu unaenda kuboresha sekta ya biashara kati ya Kenya na Tanzania na Mashirika haya Posta yatumike kama kitivo cha biashara na zilete fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili, "amesema Dkt. Chaula

Dkt. Chaula ameongeza kuwa Mashirika ya Posta yafungue milango ya biashara kwa wananchi ili kuleta wepesi wa upatikanaji wa huduma stahiki kwa wananchi kulingana na mahitaji yao

Aidha, amelitaka Shirika la Posta nchini kwa kushirikiana na Posta zingine Afrika kulinda tamaduni zetu kwa kuendelea kuipa kipaumbele lugha ya Kiswahili kwa lengo la kukuza na kutumika kama fursa kwa wafanyabiashara ili kuleta tija kwa Taifa

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema ni vema kujifunza kwa kushirikiana na wanapotoka nje ya Afrika Mashariki kuwa wamoja ili kuleta manufaa ya kuwa pamoja.

Ameongeza kuwa, zinapotokea fursa wanapaswa kwenda kama Washirika kutoka Afrika Mashariki na kuendelea kusisitiza taasisi hizi kuona umuhimu wa kuendelea kufanya tafiti ili kuleta maendeleo kwani tafiti zitawasaidia kuongeza maarifa, uelewa na kuongeza ubunifu katika kuhudumia wananchi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari amemshukuru Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Dan Kagwe kwa kuja kutembelea Tanzania na kujionea maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Posta Tanzania.

Naye, Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Daniel Mbodo, ameeleza mikakati ya Shirika la Posta nchini katika kukuza mahusiano kati yake na Posta nyingine Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, lengo ikiwa ni kurahisisha huduma za kiposta Barani Afrika

Bw. Mbodo amesema,  kuwa sasa Posta ni zaidi ya barua kwani  Shirika linaendelea kuboresha huduma zake na kuzitanua zaidi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwa Posta ya mfano katika Bara la Afrika

Kaimu Postamasta Mkuu ameongeza kuwa kutokana na maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Shirika la Posta nchini, wanatarajia kupokea ugeni kutoka nchi mbalimbalimba za Afrika ikiwemo Kongo Brazzaville,  Zimbabwe, Oman na nchi zingine za Afrika.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Dan Kagwe ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mapokezi makubwa na ushirikiano mkubwa aliopata katika ziara yake ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika Shirika la Posta Tanzania

Vilevile, Bw. Kagwe ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha na kuimarisha Sekta ya Posta nchini ili kuhakikisha linatoa huduma stahiki kwa wananchi na kwa kutumia mifumo ya kidijitali inayofanya wananchi wengi wanahudumiwa kwa wakati mmoja

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Kagwe ametoa mwaliko kwa Viongozi wa Shirika na Wizara kutembelea Kenya ili kuendelea kujenga mahusiano na kubadilishana uzoefu ili kuhudumia jamii zetu.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amekabidhi zawadi kwa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw.  Dan Kagwe pamoja na maafisa waandamizi walioongozana naye.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo na Postamasta Mkuu kutoka Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizarani, Mamlaka ya Mawasiliano na Shirika la Posta Tanzania.