Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. CHAULA AANZA UTEKELEZAJI MABORESHO YA MIFUMO YA TEHAMA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainabu Chaula leo amefungua kikao cha wadau wataalamu wa TEHAMA kutoka katika Wizara na taasisi za Serikali ili kujadili na kufanya tathmini ya mifumo ya TEHAMA inayotumika nchini ili kupata idadi, aina ya mifumo hiyo, taarifa zinazohusu mifumo hiyo na inapohifadhiwa

 

Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo jijini Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile ya kuitisha kikao hicho ili wataalamu wa TEHAMA waifanyie tathmini mifumo hiyo hasa ya kifedha ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa.

 

“Ninyi ndio wataalamu wa mifumo hivyo naamini kikao hiki kitakuwa na matokeo kwa kutafuta majibu sahihi ya maeneo yote aliyoelekeza Waziri mwenye dhamana kuhusu hii mifumo ya TEHAMA, Serikali ipo macho inaangalia na inamjua kila mtumishi na utendaji wake hivyo tusaidiane tufanye kazi kwa wema, kwa kuwa wapenda haki; wakweli na wenye uchungu na nchi yetu”, alizungumza Dkt. Chaula

 

Aliongeza kuwa taarifa zote za Wizara na taasisi za Serikali zinatakiwa kuhifadhiwa katika Kituo cha Taifa cha kuhifadhi Data (NIDC) ndio sababu ya kuundwa kwake na ndio maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Rais – Ikulu hivyo kikao chenu kichambue na kutoa taarifa sahihi ya taasisi ngapi taarifa zao zipo NIDC na zipi hazipo na kwa sababu gani.

 

Aidha, Dkt Chaula amewataka wataalamu hao pamoja na kuainisha mapendekezo ya kuboresha mifumo hiyo wanatakiwa kutengeneza utaratibu utakaozingatiwa kuhusu mifumo ya TEHAMA, kwasababu ikitumika vibaya na kuharibu mambo ni uhalifu kwasababu itakuwa imeenda kinyume na utaratibu.

 

Naye, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku amesema kuwa wajumbe wa kikao hicho ni wataalamu wa TEHAMA kutoka katika taasisi na Wizara zinazohusika na mifumo ya TEHAMA nchini na kwa pamoja wamepokea maelekezo ya Dkt. Chaula na kuyafanyia kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri wa Wizara hiyo kuhusu mifumo ya TEHAMA na kuwasilisha taarifa yao ndani ya muda uliopangwa.

 

Wataalamu hao wa TEHAMA waliokutana kwenye kikao hicho ni kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Uutmishi wa Umma na Utawala; Wizara ya Fedha na Mipango; Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Shirika la Mawasiliano Tanzania; Kituo cha Kuhifadhi Data cha Taifa; Mamlaka ya Mapato Tanzania; na Mamlaka ya Serikali Mtandao