Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Miradi ya Maendeleo Yaibadili Kongwa, Wananchi Wanufaika na Uwekezaji.


Na Mwandishi Wetu, Kongwa

Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Kongwa Julai 24, 2026, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Mkoa wa Dodoma, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), alisema hadi Juni 2026, fedha hizo Shilingi Bilioni 38.6 zilielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya sekta za afya, elimu, kilimo, skimu za umwagiliaji pamoja na miundombinu mingine ya maendeleo ili kuboresha ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.

Mhe. Kairuki alisema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu ambapo Serikali imetoa shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuboresha huduma za elimu wilayani humo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.4 la fedha zilizotengwa kwa sekta hiyo. 

Alieleza kuwa shule mpya 14 zimejengwa, huku akiahidi kutoa kompyuta 44 kwa shule mbili za wilaya hiyo na kusaidia ujenzi wa madarasa yenye miundombinu ya TEHAMA, hatua itakayowezesha wanafunzi kupata ujuzi wa kidijitali na kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Akizungumzia huduma ya maji, Mhe. Kairuki alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Soiti, Masena na Mbegio, huku ikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu kwa maeneo ambayo bado yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Aidha, alisema Serikali imejenga minara 47 ya mawasiliano wilayani Kongwa, hatua iliyoongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kufungua fursa za biashara, elimu na huduma za kidijitali. Aliongeza kuwa tathmini inaendelea katika maeneo ambayo bado yana changamoto za mawasiliano ili yaweze kufikiwa na huduma hizo kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki aliipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuanzisha huduma za Kliniki za Ardhi, akisema mpango huo umeendelea kusaidia wananchi kutatua migogoro ya ardhi kwa haraka na kupata huduma kwa urahisi.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kusikiliza kero za wananchi na kuzielekeza kwenye ufumbuzi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.