Habari
ELIMU YA USALAMA WA MTANDAO YAWAJENGEA WANAFUNZI UWEZO WA KUJIKINGA DHIDI YA UHALIFU MTANDAONI.
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Nzuguni, Dodoma
Wanafunzi kutoka Shule za Sekondari za Ursula na Lukundo zilizopo jijini Dodoma leo wametembelea Banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, ambapo wamepatiwa elimu kuhusu huduma mbalimbali za TEHAMA, hususan matumizi salama ya teknolojia na namna ya kujikinga dhidi ya uhalifu wa mtandaoni.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Charles Liwongwe amewahamasisha wanafunzi kuzingatia Usalama wa mtandao wanapotumia simu janja, kompyuta na vifaa vingine vya kielektroniki kwa kujifunzia . Amewasisitiza kutofungua viunganishi, kutowapa watu wasiowafahamu taarifa zao binafsi na kutotoa nywila za vifaa au akaunti zao.
Aidha, wanafunzi hao walipata ufafanuzi kutoka kwa Afisa TEHAMA Bw. Stanley Maliwa kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na umuhimu wake katika kurahisisha upatikanaji wa Huduma Kidigitali ikiwemo maombi ya barua ya utambulisho wanazoweza kuzihitaji watakapojiunga na vyuo.
Bw. Liwongwe aliongezea kuwa kuwafikia wanafunzi kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane ni sehemu ya juhudi za kujenga jamii yenye uelewa wa matumizi salama ya teknolojia na kuongeza uwezo wa vijana kutumia fursa za uchumi wa kidijitali kwa usalama na tija.
Kwa upande mwingine, Wanafunzi walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema itawasaidia kutumia teknolojia kwa usalama zaidi wakati wa masomo na katika shughuli nyingine za kila siku, huku wakiahidi kuwashirikisha wenzao maarifa hayo wanaporejea shuleni.
Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu Huduma na Mifumo mbalimbali ya TEHAMA sambamba na kuongeza uelewa wa matumizi salama ya teknolojia kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
