Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

CHANGAMOTO YA MAWASILIANO KITUO CHA AFYA SANGABUYE KUTATULIWA


ILEMELA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amefika katika kata ya Sangabuye iliyopo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza na kutembelea Kituo cha afya cha Sangabuye na kukuta kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Sangabuye amesema kuwa eneo ambalo mtandao unaweza kupatikana vizuri ni eneo la Kayenze, lakini eneo la kituo hicho halina mawasiliano kabisa mpaka uteremke ziwani ndio kidogo mawasiliano yanapatikana kwa shida

Amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo machache ukiwa nje ndio mawasiliano yanapatikana kitu kinachowafanya kutoka ofisini na kwenda kusimama katika maeneo yenye mawasiliano ili kuweza kuwasiliana na Hospitali ya Seketure au Bugando iwapo kuna mgonjwa anayehitaji kupewa rufaa ya matibabu

Amesema kuwa kutokana na changamoto ya mawasiliano wanashindwa kuthibitisha uhalali wa bima za afya zinazotumiwa na wagonjwa kwa wakati kwasababu ya changamoto ya mtandao lakini kutokana na uharaka wa kuwahudumia wagonjwa inawalazimu kumhudumia mgonjwa ili awahi kuondoka lakini meseji ya taarifa za bima zinaporudi inaweza kuwa bima inatumika au imesitishwa

Mhandisi Kundo baada ya kusikia changamoto hiyo alisema kuwa hali hiyo inatia hofu na mashaka kwasababu shughuli nyingi za kitabibu katika vituo vya afya haziwezi kufanyika kwa kiwango kinachotakiwa iwapo kunakuwa na changamoto ya mawasiliano ukizingatia shughuli nyingi zinafanyika kwa kutumia mifumo ya TEHAMA ambayo inatumia mtandao.

Amesema kuwa hali hiyo haijakaa vizuri kwa usalama na afya za wananchi katika eneo hilo la kata ya Sangabuye kwasababu huduma ya mawasiliano ni haki ya msingi kwa wananchi lakini pia mawasiliano ni usalama, mawasiliano ni uchumi na mawasiliano ni nyenzo muhimu ambayo inaweza kuokoa maisha ya watu kwa kurahisisha ufikishaji wa taarifa sehemu husika kwa ajili ya dharura ikiwemo dharura ya wagonjwa

Kutokana na umuhimu wake Mhandisi Kundo amesema kuwa amefanya majadiliano na taasisi za mawasiliano za TCRA, UCSAF na TTCL ambapo wamemuhakikishia kuwa watafuata maelekezo yake na kuahidi ndani ya miezi sita huduma ya mawasiliano itakuwa imefikishwa katika kata hiyo ya Sangabuye hasa katika eneo la kituo hicho cha Afya kwa kujenga mnara wa mawasiliano