Habari
BURUNDI WAJIFUNZA TANZANIA KURATIBU MAWASILIANO NA TEHAMA

Naibu Katibu Mkuu Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa ameikaribisha Timu ya Wataalam kutoka Mfuko wa Huduma za Mawasiliano kwa Wote (USF) wa Burundi waliofika nchini kwa ajili ya kujifunza namna ya kuratibu na kusimamia masuala ya Mawasiliano na TEHAMA.
Akizungumza na Ujumbe huo katika Ofisi za Wizara leo Machi 20, 2025 Bw. Mkapa amewakaribisha wataalam hao kujifunza zaidi na kwamba wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake iko tayari kutoa ushauri katika maeneo yanayohusu huduma za mawasiliano.
Naye kiongozi wa Ujumbe huo kutoka Burundi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Huduma za Mawasiliano kwa Wote (USF) Bw. Elias Ahiboneye amesema kuwa lengo la ziara yao ni kuja kujifunza kwa Tanzania ni kwa namna gani wameweza kuboresha mawasiliano katika jamii na huduma TEHAMA.
Bw. Ahiboneye aliongeza kuwa Taasisi hiyo ya USF ina mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwake hivyo kupitia ziara hii USF itakwenda kuweka mipango mizuri zaidi itakayowezesha wananchi wote kupata huduma za mawasiliano bila vikwazo vyovyote.
Wataalam hao kutoka Burundi walifika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakitokea Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ikiwa ni muendelezo wa ziara yao hapa nchini ambapo kesho wanatarajia kutembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kituo cha Taifa cha Kutunza Data (NIDC) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).