Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

BILIONI 134 ZAWEKEZWA KWENYE SEKTA YA MAWASILIANO MWEZI SEPTEMBA 2023


Na Innocent Mungy

Ndani ya kipindi kifupi cha mwezi mmoja wa Septemba 2023, Sekta ya Mawasiliano nchini imefanikiwa kuwekeza kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 134. Fedha hizi zinawekezwa kwenye Sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi, ili kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
 
Mafanikio haya makubwa, yametokana na utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais, alielekeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kuwa inaendelea kuunganisha nchi majirani na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
 
Katika kutekeleza agizo hilo Wizara  ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ndani ya Mwezi Septemba kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania {TTCL} imesaini mikataba ya kibiashara kati ya Jamhuri ya Malawi na Jamhuri ya Uganda, kufuatia zira za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu hassan kufanya ziara katika nchi hizo na kukutana na Marais wa nchi hizo. 
 
Mkataba kati ya Tanzania na Uganda wa kutumia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano una thamani ya Shilingi za Kitanzania bilioni 71.7. Mkataba kati ya Malawi na Tanzania wa kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano una thamani ya Shilingi za Kitanzania bilioni 13.5. Jumla ya fedha hizi ni shilingi bilioni 84 za Kitanzania.
 
Katika hatua nyingine Mhe. Rais aliagiza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya Serikali na watoa huduma za Mawasiliano nchini utatuliwe ili kazi ya kuendelea kuboresha huduma za Mawasiliano nchini iendelee kwa kasi inayotakiwa. Hii ni kulingana na falsafa yake ya Maridhiano, Uvumilivu, Mageuzi na Kujenga Upya nchi (4R’s - ). 

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kutekeleza maagizo hayo, mwezi Septemba imekamilisha mazungumzo na watoa huduma {Consortium of Telecom operators} na kusaini maridhiano na nyongeza ya Mkataba ambayo thamani yake ni Shilingi za Kitanzania bilioni 50. Aidha, Watoa Huduma hao wameahidi kuwekeza Shilingi bilioni 32.5 katika maendeleo ya miundombinu zaidi nchini.
 
Matukio haua matatu ndani ya Mwezi mmoja zimevutia Jumla ya kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 134 Kwenye Sekta ya Mawasiliano na zingine bilioni 32.5 zitawekezwa na Makampuni moja kwa moja kwenye Sekta ya Mawasiliano. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye katika tukio la kusaini makubaliano kati ya Tanzania na Uganda alisema anatamani kuona Tanzania inaiunganisha Afrika kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchini. Aidha aliitaka Bodi na Menejimenti ya Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi makubaliano Haya ya kibiashara na hategemei kusikia malalamiko kutoka kwa nchi hizo mbili.

Haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.