Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ANWANI ZA MAKAZI, SENSA YA WATU NA MAKAZI KUSAIDIA UFIKISHAJI WA HUDUMA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohamed Khamis Abdulla (mwenye suti) akikagua kibao cha Anwani ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa zoezi la Anwani za Makazi katika mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar

 

ZANZIBAR

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla ameainisha faida za Anwani za Makazi pamoja na zoezi la sensa ya watu na makazi kuwa ni pamoja na kurahisisha ufikishaji wa huduma za kijamii na kiuchumi mathalani majanga ya njaa na mafuriko iwapo yakitokea Serikali itahitaji kutambua idadi ya watu ili kuwafikishia huduma kulingana na uhitaji

Akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Bwana Abdulla amesisitiza watendaji kuongeza kasi ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi ili kukamilisha kwa muda uliopangwa na Serikali

Amesema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti mwaka huu linategemea Mfumo wa Anwani za Makazi ili kuwarahisishia wale watakaofanyakazi ya kuhesabu watu kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa sensa ya mwaka huu itafanyika kidijitali kupitia mfumo huo wa utambuzi wa wakazi na makazi

Katika ziara hiyo, Bwana Abdulla amefanikiwa kutembelea na kuona baadhi ya majina ya mitaa yaliyowekwa kwa marumaru “marbles” na namba za nyumba zilizokuwepo toka enzi za mkoloni katika mitaa ya Mji Mkongwe uliopo katika mkoa huo ambazo zitaendelea kutumika na tayari zimeshaingizwa kwenye mfumo wa utambuzi wa NaPA

Aidha, nguzo zenye majina ya barabara zitawekwa kwenye barabara 11 za makutano katika maeneo mbalimbali ya Mamlaka ya Mji Mkongwe na marumaru 180 zenye majina ya mitaa zitawekwa kwenye mitaa ambayo haina ili kukamilisha zoezi la uwekaji wa miundombinu hiyo

Kama tunavyofahamu, Februari 8, mwaka huu wa 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alitangaza utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi kuwa operesheni maalumu kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 28 kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar  

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kukagua, kuhamasisha, kusimamia na kusaidia utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi kupitia wataalamu waratibu waliopelekwa katika kila mkoa pamoja na ziara zinazofanywa na viongozi wa Wizara hiyo ili kuhakikisha kila mkoa unafikia lengo na matarajio ya Serikali ya kukamilisha kabla ya Mei 22 mwaka huu