Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI KUONGEZA TIJA BIASHARA MTANDAO


 

 

Mahitaji ya uwekaji wa miundombinu ya anwani za makazi na postikodi yanazidi kuongezeka nchini kutokana na kurahisisha kufanyika kwa biashara mtandao na kukuza uchumi wa kidijitali kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndio inayotekelezwa na Serikali katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2020 – 2025.

 

Hayo yamezungumzwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew katika baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo ambalo lilianza kwa watumishi wote kujengewa uelewa wa Mpango wa uwekaji wa Anwani za Makazi na Postikodi nchini.

 

Aliongeza kuwa kama nchi tunahitaji miundombinu ya anwani za makazi na postikodi inayotambulisha namba ya kanda, mkoa, wilaya, kata, jina la mtaa/barabara na namba ya nyumba itakayowezesha mwananchi kuagiza bidhaa kwa njia ya mtandao na bidhaa hiyo kumfikia mahali alipo.

 

Aidha, amesema kuwa, mawasiliano yanaenda kuwa moja ya njia kuu ya kukuza uchumi wa nchi ambapo kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Serikali inakusanya bilioni 80 kwa mwezi kama tozo ya miamala inayopita kwenye mitandao na kiasi cha shilingi trilioni 18 zinapita katika mitandao ya simu kwa mwezi ikiwa ni matokeo ya kuwepo kwa miundombinu bora inayotoa huduma za mawasiliano na TEHAMA.

 

Kwa upande mwingine Mhe. Mhandisi Kundo amesema kuwa Wizara ipo katika mchakato wa kuandaa sheria ya TEHAMA ili kama nchi tuwe na sheria mahususi itakayotoa muongozo wa kisheria juu ya masuala ya TEHAMA ili Wizara na taasisi zote ziweze kufuata kwa matumizi yenye tija kwa nchi.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa uwekaji wa anwani za makazi na postikodi ni kipaumbele cha Serikali kupitia Wizara hiyo na utekelezaji wake ni shirikishi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

 

Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imewekeza katika kuboresha Mkongo wa Taifa wa mawasiliano ambapo kiasi cha shilingi bilioni 8 zilitengwa na Serikali kuhakikisha maboresho hayo yanafanyika na mpaka sasa Wizara ipo katika hatua za utekelezaji.