Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ANWANI ZA MAKAZI KUWA KIPIMO CHA UTENDAJI KWA WATENDAJI WA SERIKALI ZA MITAA


Watendaji wa Serikali za Mitaa wametakiwa kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi ni endelevu na wenye tija kwa kuwa mfumo huo ni daftari la kidijitali la wakazi na makazi litakalowezesha viongozi na watendaji kufuatilia maendeleo, kutoa huduma kwa haraka na kupunguza gharama za ukusanyaji wa taarifa.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Adolf Ndunguru, na kuwasilishwa na Bw. Christopher Kafunga, Mchumi kutoka Ofisi hiyo leo Septemba 24 wakati wa kuhitimisha mafunzo ya zoezi la uhakiki wa taarifa za mfumo wa Anwani za Makazi kwa watendaji wa kata na mitaa katika jiji la Mbeya.

Ameongeza kuwa zoezi la kuhakiki taarifa za Anwani za Makazi litakuwa kipimo cha utendaji kazi wa watendaji wote wa Serikali za Mitaa hivyo wanapaswa  kulipa uzito mkubwa zoezi hilo na kujitoa kwa hali na mali ili kufanikisha utekelezaji wake.

Bw. Kafunga amesisitiza kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi ni hatua ya kimageuzi katika usimamizi wa maeneo ya kiutawala na utarahisisha utambuzi wa wakazi wote pamoja na shughuli zao.

Amesema kupitia mfumo huo, huduma nyingi za Serikali za Mitaa zitatolewa kidijitali, ikiwa ni pamoja na utoaji wa barua za utambulisho wa wakazi zinazotolewa kupitia Mfumo wa NaPA 

“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu, unaongeza ufanisi na unapunguza gharama za Serikali na pia ni msingi wa huduma nyingi zinazotolewa na TAMISEMI kuanzia utambuzi wa kaya maskini, kaya zenye mahitaji maalum, hadi ufuatiliaji wa maendeleo”, amesema Kafunga.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi na viongozi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha taarifa zote za Anwani za Makazi zinahakikiwa na kusasishwa ipasavyo, ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

​​​​​​​