Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ANWANI ZA MAKAZI KUCHAGIZA UCHUMI WA KIDIJITI – DKT. YONAZI


Leo Juni 30, 2022 Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi ametembelea kituo cha redio cha AFM 92.9 jijini Dodoma na kutolea ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi, Usalama wa taarifa binafsi za wananchi na matumizi salama ya mtandao

Dkt. Yonazi amezungumzia mfumo wa utambuzi wa Anwani za Makazi kuwa unahusisha postikodi, namba ya nyumba na jina la barabara na mtaa, ambapo mfumo huo ulikuwa ukitekelezwa toka mwaka 2010, lakini msukumo mkubwa umekuja wakati ambapo Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa kidijiti

Aidha, ameuzungumzia uchumi wa kidijiti kuwa ni uchumi ambao unafungua fursa nyingi za biashara na wananchi wanaweza kushiriki kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kama vile simu ya mkononi, televisheni, redio na kompyuta na ili uchumi huu uwe shirikishi ni lazima kuwa na mfumo wa utambuzi ili kujua mahali huduma zilipo na namna ya kumfikia mwananchi

Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijiti pamoja na zoezi la sensa ya watu na makazi linaloenda kufanyika Agosti 23 mwaka huu ndio uliongeza msukumo zaidi wa utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ambapo Rais Samia alielekeza utekelezwe kwa njia ya operesheni ili kabla ya sensa mfumo wa utambuzi wa Anwani za Makazi uwe umekamilika ambao utarahisisha zoezi zima la sensa lakini pia ufikishaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na kibiashara kwa mwananchi

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameizungumzia TEHAMA kuwa nyenzo muhimu kwenye uchumi wa kidijiti pamoja na kufungua fursa nyingi za uzalishaji na biashara lakini pia TEHAMA inaweza kutumika na watu wasio na nia njema kufanya uhalifu, hivyo amewataka wananchi kuwa makini wasifanye kitu chochote mtandaoni bila kujiridhisha uhalali wa jambo husika

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo inaendelea kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa taarifa binafsi kwa kuandaa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi lakini pia Wizara hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya matumizi salama ya mtandao ikiwa ni pamoja na ulinzi wa taarifa binafsi.