Habari
ANWANI YA MAKAZI KURAHISISHA UPOKEAJI NA UTOAJI HUDUMA NA BIDHAA
Na Immaculate Makilika – WHMTH
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wadau washirika inaratibu utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003, makubaliano ya kikanda kupitia Umoja wa Posta Afrika, makubaliano ya kimataifa kupitia Umoja wa Posta Duniani na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025.
Akizungumza juzi (Januari 10, 2023), katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi iliyopo mkoani Morogoro wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa redio TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi unaharakisha na kurahisisha upatikanaji, utoaji na ufikishaji wa huduma hadi mahali stahiki na kuwa ni nyenzo muhimu katika kuwezesha uchumi wa kidijitali.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na anwani ya makazi katika eneo lake la nyumbani, ofisini ama eneo la biashara ili kuongeza tija na ufanisi wa shughuli za kijamii na kiuchumi”. Ameeleza Naibu Waziri huyo, Mhe. Mhandisi Kundo.
Aidha, amefafanuwa manufaa ya Anwani za Makazi ambapo sasa utekelezaji wake umezifikia shehia, mitaa na vijiji vyote nchini kuwa ni kuimarisha ulinzi na usalama, kurahisisha ufikishaji wa huduma na bidhaa hadi mahali stahiki yaani nyumbani, ofisini ama eneo la biashara na kuwezesha kufanyika kwa biashara mtandao.
Vilevile, faida zingine zinatajwa kuwa ni kuongeza ajira hususan za kufikisha huduma na bidhaa hadi mahali stahiki, kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla.
Itakumbukwa kuwa utekelezaji wa zoezi la Anwani za Makazi umepata msukumumo mkubwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Februari 08, 2022 ya kutaka utekelezaji wa mfumo huo ufanyike kwa njia ya operesheni chini ya usimamizi wa Wakuu wa Mikoa na kukamilika mwezi Mei, 2022. Ambapo maelekezo hayo yalilenga kuwezesha nchi kuanza kupata manufaa mapana ya mfumo pamoja na kuweka msingi wa Sensa ya Watu na Makazi ambayo ilifanyika Agosti, 23 Agosti hadi 05 Septemba, 2022.
Pia, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na wadau washirika wakiwemo Wakuu wa Mikoa iliratibu kwa mafanikio makubwa utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi ambao hadi kufikia Mei 31, 2022 utekelezaji wake ulifanyika kwa zaidi ya asilimia 95.