Habari
AFD YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA SERIKALI KUWEZESHA MAENDELEO YA KIDIJITALI NCHINI

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) nchini Tanzania, Bi. Céline Robert, kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Kidijitali.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Oktoba 7, 2025 katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba, yalilenga kujadili namna AFD itakavyosaidia kufanikisha mpango huo unaofadhiliwa na shirika hilo kama msaada (grants) wenye thamani ya Euro 500,000.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi. Robert alisema AFD ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya kidijitali, kwa kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji ushirikiano mpana na uratibu wa karibu kati ya wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kwa upande mwingine, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka kampuni ya Tactis, alisema upembuzi yakinifu wa awali wa mradi huo unaendelea vizuri licha ya changamoto ya ucheleweshaji wa majibu kutoka kwa taasisi mbalimbali na malengo ni kukamilika upembuzi huo katikati ya Novemba 2025.
Katibu Mkuu Abdulla alieleza kuwa dira ya Serikali kupitia Wizara hiyo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, kila eneo nchini kuwa limeunganishwa na huduma za mawasiliano ya kidijitali.
“Tunataka kuwa na Serikali inayomgusa mwananchi moja kwa moja, ambapo kila mwananchi ataweza kutumia simu janja au kifaa kingine cha kidijitali kupata huduma zote za Serikali,” alisema.
Aidha, alitoa rai kwa AFD kuangalia pia uwezekano wa kusaidia maeneo ya teknolojia zinazoibukia pamoja na mafunzo kwa wataalamu watakaotekeleza mradi huo.
Kwa ujumla, pande zote mbili zimeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kuwa taifa lenye uchumi wa kidijitali.