Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA YASAINI MAKUBALIANO NA KAMPUNI YA EXTENSIA YA UINGEREZA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (Kulia) na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Extensia Limited, Bw. Tariq Malik wakitia saini Mkataba wa Makubaliano wa kuandaa Kongamano litakalowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano wa ndani na nje ya nchi linalojulikana kama Connect To Connect, tukio lililofanyika leo Julai 25, 2022 jijini Dodoma.

DODOMA.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesaini mkataba wa makubaliano na kampuni ya Extensia Limited ya Uingereza, lengo likiwa ni kuandaa Kongamano litakalowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano wa ndani na nje ya nchi linalojulikana kama Connect To Connect.

Kongamano hilo pia linalenga kuzidi kukuza matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufungua wigo wa mifumo, ubunifu na uwekezaji katika TEHAMA.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema  Kongamano la Connect To Connect (C2C) litafanyika kwa siku mbili tarehe 7 na 8 Septemba, 2022 ambapo nchi nyingi zinatarajiwa kushiriki ikiwa ni pamoja na nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki.

Amesema kuwa Tanzania inaunganisha nchi saba za jirani ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na Msumbiji  kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo kuwa na fursa kubwa ya kupeleka huduma na kuchichimua uchumi kupitia TEHAMA.

Dkt. Yonazi ameeleza kuwa Kongamano litatoa pia fursa kwa nchi zitakazoshiriki kufanya majadiliano, kujifunza na kuweka mikakati ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuchangia uchumi , kuongeza fursa za uwekezaji, ajira na elimu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Extensia Limited, Bw. Tariq Malik amesema kuwa Kongamano hilo lilifanyika Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 na kuleta mafanikio makubwa. Aidha, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano kwa mara nyingine ambapo itapaisha zaidi Tanzania kama kitovu cha mawasiliano.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku amesema kuwa utiaji saini wa makubaliano hayo ni hatua ya awali ya kuanza maandalizi ya Kongamano kubwa litakalowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano zaidi ya 300 kutoka ndani na nje ya nchi.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Habari- MAELEZO,Bw. Gerson Msigwa ameipongeza Wizara kwa juhudi za kuweka mifumo imara ambayo itasaidia kutimiza malengo ya Serikali ya kuinua uchumi wa nchi kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.